Guinea ya Ikweta yatoa wito kwa taasisi za haki za binadamu
19 Aprili 2018Guinea ya Ikweta imetoa mwito kwa taasisi za haki za binadamu za kitaifa barani Afrika kuchukua nafasi ya shughuli zinazofanywa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu barani humo.
Hatua hiyo inakuja baada ya serikali ya nchi hiyo kukosolewa kufuatia operesheni yake iliyofanyika baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana.
Rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Teodoro Obiang Nguema alisema wakati wa kuanza kwa mkutano wa kilele katika mji mkuu wa nchi hiyo Malabo kuwa atapendekeza kuanzishwa kwa taasisi za haki za binadamu katika kila nchi barani Afrika.
Taasisi za aina hiyo tayari zipo katika mataifa mengi barani Afrika ikiwa ni pamoja na mahakama ya haki za binadamu ya Afrika iliyoko nchini Tanzania.
Hata hivyo Obiang ambaye amelitawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1979 anataka shughuli za haki za binadamu ziendeshwe na mashirika ya nchi za Afrika akisema mashirika ya haki za binadamu ya kimataifa yana malengo ya kuyasambaratisha mataifa ya Afrika kama inavyoonekana kwa Guinea ya Ikweta.