1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea yatangaza kukumbwa na mlipuko mpya wa Ebola

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
14 Februari 2021

Serikali ya Guinea imesema kuwa watu saba wamethibitishwa kuwa wameambukizwa Ebola katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambapo watatu kati yao tayari wamefariki dunia.

Kongo: Erneuter Ausbruch von Ebola
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Afisa mkuu wa idara ya Kitaifa ya Afya nchini Guinea Daktari Sakoba Keita alisema baada ya mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Conackry kwamba watu saba wamethibitishwa kuwa wameambukizwa Ebola katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambapo watatu kati yao tayari wamefariki dunia. Watu wanne ambao bado wako hai wametengwa kwenye vituo maalum.

Idara ya afya ya taifa imesema watu hao walianza kuugua huku wakiendesha, kutapika na kuvuja damu baada ya kuhudhuria mazishi kwenye wilaya ya Goueke. 

Idara hiyo pia imeongeza kusema kuwa awamu nyingine ya vipimo inaendelea ili kuthibitisha maambukizi hayo ya virusi vya Ebola na wafanyakazi wa huduma za afya tayari wanawafuatilia watu wote waliokutana na wagonjwa hao

Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) nchini Guinea Alfred George Ki-Zerbo amesema shirika hilo litapeleka msaada haraka kusaidia Guinea, ambayo tayari ina uzoefu mkubwa wa kutibu ugonjwa huo wa Ebola.

Rais wa Liberia George WeahPicha: picture-alliance/A.Dulleh

Wakati huo huo katika nchi jirani ya Liberia rais George Weah ametangaza kuziweka mamlaka za afya za nchi hiyo katika kiwango cha juu cha tahadhari baada ya watu kufariki dunia kwa ugonjwa wa Ebola kwenye taifa jirani la Guinea.

Weah ameamuru mamlaka za afya za Liberia na wadau wengine kuongeza ufuatiliaji wa karibu wa hali inayoendelea pamoja na kuchukua hatua za udhibiti kufuatia ripoti za kuzuka upya homa ya Ebola nchini Guinea.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia imekabiliwa na mlipuko wa Ebola ambapo shirika la afya duniani WHO mnamo siku ya Alhamisi ilithibitisha kuzuka tenaugonjwa huo miezi mitatu baada ya nchi hiyo kutangaza kumalizika kwa ugonjwa huo.

Nchi hiyo ilikumbwa na milipuko mara 11 ya Ebola iliyosababisha vifo vya watu 55 kati ya watu 130 walioambukizwa.

Zoezi la chanjo ya Ebola katika eneo la Mbandaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mnamo mwaka 2018Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Tamko la serikali ya Guinea-Conackry

Tamko la serikali ya Guinea kuhusu mlipuko wa Ebola limetolewa wiki moja baada ya eneo la mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuthibitisha kuwa wapo watu walioamukizwa ugonjwa huo ingawa maambukizi hayo hayaunganishwi kwa pamoja.

Wataalam wa afya nchini Guinea wamesema maambukizi haya mapya yaliyojitokeza hivi karibuni yanaweza kuwa makubwa na hivyo kulirudisha nyuma taifa hilo masikini, ambalo kwa sasa linapambana na COVID-19.

Guinea bado inaendelea kujikongoja kutokana na mlipuko wa awali wa Ebola, ambapo watu wapatao  2,500 walikufa.  Wakati wa mlipuko huo katika miaka ya 2014 na 2016,  zaidi ya watu 11,000 walikufa kwenye mataifa ya Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Wataalam wa afya wanatumai kuwa kupatikana kwa chanjo ya Ebola kutasaidia kudhibiti haraka mlipuko huu. Ebola inaambukiza kupitia mawasiliano ya moja kwa moja ya maji maji ya mwili kutoka kwa mtu anayeonyesha dlili za ugonjwa huo au kutoka kwenye  maiti za watu waliokufa na ugonjwa huo wa Ebola.

Mwezi uliopita Shirika la Afya Ulimwenguni WHO lilisema limeunda akiba ya dharura ya takriban dozi 500,000 za chanjo za Ebola lakini ni chanjo 7,000 tu zilizopo wakati huu wa taarifa ya kuzuka kwa mlipuko huo. Chanjo hiyo ya Ebola imetengenezwa na kampuni ya Merck ya New Jersey nchini Marekani.

Vyanzo:/AP/AFP/RTRE