1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guteress awatolea wito viongozi wa G20 kuhusu COP29

18 Novemba 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa awatolea wito viongozi wa G20 kufanikisha mazungumzo ya COP29.

Guterres akihutubia mkutano wa COP29 mjini Baku, Azerbaijan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano wa COP29 mjini Baku, AzerbaijanPicha: Sean Gallup/Getty Images

Antonio Guterres amewatolea wito viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani wa G20 waliokusanyika nchini Brazil, kufanikisha mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa ya COP29 yanayoendelea nchini Azerbaijan.

Guterres, ambaye atahudhuria mkutano wa kilele wa G20 unaoanza hivi leo huko Rio de Janeiro, amesema matokeo yenye mafanikio katika COP29 bado yanaweza kufikiwa, lakini yatahitaji uongozi na maelewano kutoka kwa nchi za G20.

Soma pia: G20 yahimizwa kutanzua mkwamo wa mazungumzo ya COP29

Mazungumzo ya COP29 mjini Baku yamekwama licha ya wiki moja ya majadiliano, huku mataifa yakishindwa kuafikiana mkataba wa dola trilioni 1 kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya hali ya hewa katika mataifa yanayoendelea.

Mbali na kiwango hicho, bado kuna mivutano pia kuhusu aina ya ufadhili na nani anayepaswa kutoa fedha hizo, huku nchi za Magharibi zikiitaka China na mataifa tajiri ya Ghuba kujiunga katika orodha ya wafadhili.