1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aapa kukisaidia kikosi cha G5 Sahel

Josephat Charo
31 Mei 2018

Katika Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameahidi (30.05.2018) kukisaidia kikosi kinachopambana na ugaidi katika eneo la Sahel, licha ya hatua ya Marekani kupunguza mchango wake wa kifedha kwa umoja huo.

Mali Besuch UN Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: Getty Images/AFP/S. Rieussec

Guterres aliyatembelea makao makuu ya kikosi kinachojulikana kama G5 Sahel jana katika mji wa Sevare, siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake nchini Mali, nchi inayopambana na uasi wa wanamgambo katika eneo la Sahel.  Katika ziara yake katika tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa inayoelezwa kuwa hatari kabisa nchini humo, MINUSMA, Guterres pia alikutana na viongozi wa kidini na wa jamii mbalimbali mjini Mopti, katikati mwa Mali, pamoja na maafisa wa tume hiyo.

Guterres alisema, "Naamini kwamba eneo la katikati mwa Mali leo ni ufunguo muhimu katika kuutanzua mgogogoro wa Mali. Tunahitaji bila shaka kuepusha kusambaratika kwa eneo hili. Tunahitaji kuimarisha tena usalama na kurejesha hali ya kawaida katikati mwa Mali."

Katibu Mkuu huyo aidha alisema ziara hiyo imemfanya kuwa na moyo wa huruma na Umoja wa Mataifa utajitahidi kuisaidia nchi hiyo kuandaa na kufanya uchaguzi wa rais mnamo Julai 29 ambao utakuwa huru, licha ya changamoto kubwa zilizopo. Chaguzi zimekuwa zikiahirishwa mara kwa mara kutokana na hali mbaya ya usalama na wasiwasi kuhusu wanamgambo wa kiislamu wenye itikadi kali za kidini.

Ufaransa iliingilia kati kijeshi nchini Mali mnamo mwaka 2013 kuyasaidia majeshi ya serikali kuwafurusha wapiganaji wa jihadi wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda katika eneo la kaskazini. Tume ya awali ilifuatiwa mwaka 2014 na Operational Barkhane, ambayo iliwajumuisha wanajeshi 4,000 wa Ufaransa pamoja na wanajeshi 12,000 wa tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA. Hata hivyo uasi umeenea hadi maeneo ya katikati na kusini mwa nchi na kuvuka mpaka hadi nchini Burkina Faso na Niger.

Mwanajeshi wa Uholanzi wa kikosi cha MINUSMA kambi ya Gao Novemba 29, 2017.Picha: Getty Images/AFP/M. Cattani

Guterres aahidi udhamini kwa kikosi cha Sahel

Guterres na viongozi wa Ufaransa wamekuwa wakifanya ushawishi kutaka kikosi cha G5 Sahel kijengewe uwezo wa kukamilisha majukumu yake kwa wepesi na kipewe fedha zaidi na Umoja wa Mataifa, ambayo itakuwa ni njia ya ziada kuongeza msaada wa kiufundi kutoka kwa kikosi cha MINUSMA. Lakini Mei 23 mwaka huu Marekani ilisema inapinga mamlaka ya baraza la usalama kuhusu kikosi hicho na udhamini wa moja kwa moja wa kifedha kwa Umoja wa Mataifa.

Licha ya kikwazo hicho, Guterres amesema MINUSMA itaendelea kukipa kikosi cha Sahel kila aina ya msaada jinsi inatakavyowezekana, akiongeza kwamba anaunga mkono mamlaka makubwa zaidi ya baraza la usalama juu ya kikosi hicho.

"Tumependekeza aina ya udhamini wa kifedha wenye dhamana na uhakika utakaokiwezesha kikosi cha Sahel kupanga mkakati wake wa siku zijazo kwa wepesi. Hatujafaulu kuyatimiza melengo yote tuliyojiwekea, ya kukisadia na kukifadhili vyema zaidi kikosi cha Sahel," alisema Guterres.

Kikosi cha Sahel kilitarajiwa kuwa na uwezo wa kuendesha shughuli zake kikamilifu kuanzia Machi mwaka huu, lakini kimekabiliwa na hali ya kucheleweshwa na hakina vifaa madhubuti vya kisasa.

Guterres aliyatembelea pia makao ya MINUSMA hapo jana na kuwamiminia sifa kedekede wanajeshi wa tume hiyo, ambayo imekabiliwa na idadi kubwa ya vifo vya maafisa wa kulinda amani ikilinganishwa na tume yoyote nyingine ya amani ya Umoja wa Mataifa ulimwenguni.

Mwandishi: Josephatd Charo/afpe/aptn

Mhariri: Saumu Yusuf