Guterres ahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
25 Septemba 2018Akizungumzia kwa ufupi juu ya hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alisema Guterres pia atazungumzia kuhusu masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi na kusisitiza kuwa watu wote lazima wanufaike na tekinolojia mpya.
Aidha atatoa mwito kwa viongozi wa kidunia juu ya haja ya kushikamana kwa ajili ya kudumisha amani pamoja na kuheshimu haki za binadamu.
Jumla ya viongozi 133 wa dunia wanatarajia kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa utakaomalizika Oktoba 1, likiwa ni ongezeko kulinganisha na viongozi 114 waliohudhuria mkutano wa mwaka jana. Hata hivyo nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitawakilishwa katika mkutano huo na baadhi yake zikiwakilishwa na mawaziri.
Katika kuelekea mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akizungumzia dhidi ya kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo, na haja ya kufanyika mageuzi katika siasa za kimataifa hususan katika kipindi hiki ambacho hayajawahi kuhitajika kama yanavyohitajika sasa.
Trump kuhutubia mkutano huo
Viongozi wanaofuta siasa kali za kizalendo wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na rais Donald Trump wa Marekani, rais wa Poland Andrzej Duda, waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Hungary na Austria.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliwaeleza waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa rais Donald Trump anayepigia upatu sera ya " Marekani Kwanza" atazungumzia juu ya kulinda utaifa wa Marekani wakati atakapohutubia mkutano huo muda mfupi mara baada ya Guterres kutoa hotuba yake.
Wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kujadili amani sambamba na kuadhimisha miaka 100 ya kiongozi aliyeoongoza harakati za kupinga ubaguzi nchini Afrika Kusini hayati Nelson Mandela waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi alionya kuwa siasa kali za kizalendo na sera za kuyahami masoko zinazidi kuongezeka.
China na Marekani katika miezi ya hivi karibuni zimekuwa katika hali ya vita ya kibiashara huku nchi zote mbili zikitoza viwango vikubwa vya kodi kwa bidhaa kutoka pande zote mbili.
Masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale yanayohusiana na migogoro, maeneo yanayokabiliwa na wasiwasi wa kiusalama yanatarajiwa kujadiliwa pembezoni mwa mkutano huo wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Mgogoro wa Syria uliodumu miaka saba sasa, mgogoro wa Yemen uliosababisha janga la kibinadamu pamoja na maeneo mengine barani Afrika yaliyo katika wasiwasi wa kiusalama ikiwa ni pamoja na Libya, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati , Mali na Congo huenda pia yakachukua nafasi katika mkutano huo.
Mwandishi: Isaac Gamba/APE
Mhariri: Bruce Amani