1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aisifu Nigeria kwa kuwasaidia wapiganaji wa zamani

4 Mei 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameisifu Nigeria kwa mpango wake wa kuwasaidia wapiganaji wa zamani wa kundi la Boko Haram kurejea katika maisha ya kawaida akisema hilo "ni jambo jema ili kuleta amani"

New York I Generalsekretär der Vereinten Nationen Antonio Guterres
Picha: Richard Drew/AP/picture alliance

Katibu Mkuu Guterres ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la kaskazini mashariki mwa Nigeria la Borno eneo ambalo ni kitovu cha uasi wa kundi la Boko Haram kwa miongo kadha.

Guterres amesema juhudi za serikali ya Nigeria za kuwasaidia wapiganaji walioliasi kundi la Boko Haram zinapaswa kuungwa mkono kwa sababu zitasaidia kuleta amani.

Amesema iwapo watu walioamua kwenda msituni baada ya kukataa tamaa na maisha wameamua kurejea uraiani ni jambo la busara kuwapa msaada wote unaohitajika.

Jeshi la Nigeria linasema hadi sasa wapiganaji wa zamani 1,629 wamehitimu mafunzo chini ya mpango wa kuwasaidia kiujuzi na kimaadili kurejea uraiani.

Guterres aitaka Jumuiya ya Kimataifa kuipiga jeki Nigeria 

Wakati wa ziara hiyo kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa alikutana na wapiganaji wa zamani katika kambi moja inayowahifadhi na kuwapa mafunzo. Alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuiunga mkono Nigeria hususan upande wa kaskazini mashariki ambako serikali za majimbo zinakabiliwa na changamoto lukuki.

Picha: Gilbertson/ZUMAPRESS/picture alliance

‘'Kwa dhati kabisa ningependa kuirai Jumuiya ya Kimataifa kuitambua Borno kuwa jimbo la matumaini na kusaidia juhudi za kiutu kwenye jimbo la Borno. ni sharti itambue changamoto nzito ambazo jimbo la Borno inapitia, mabadiliko ya tabia nchi, na Boko Haram bado inaendesha operesheni zake japo imedhoofika. Jumuiya ya Kimataifa iwekeze kwenye jimbo la Borno lenye matumaini " amesema Guterres.

Kundi la Boko Haram lilianzisha uasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu mnamo mwaka 2009 kwa dhima ya kupinga elimu inayofuata miongozo ya mataifa ya magharibi na kuanzisha utawala wa Sharia, unafuata misingi ya kidini.

Uasi huo ulitapakaa hadi kwenye mataifa jirani ya Cameroon, Niger na hata Chad. Mwaka 2014 kundi hilo liliustua ulimwengu lilipowateka nyara wanafunzi wa kike 276 kutoka kijiji cha Chibok na hadi sasa 100 kati yao hawajulikani waliko.

Hali ya kanda ya Sahel yamtisha Katibu Mkuu Guterres 

Picha: ISSOUF SANOGO/AFP

Kabla ya ziara yake nchini Nigeria, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliitembelea Niger siku ya Jumatatu ambako alielezea wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa hujuma zinazofanywa na makundi ya itikadi kali kwenye kanda ya Sahel.

Kanda hiyo inayajumuisha mataifa 5 yaliyo kwenye eneo kame, kusini mwa jangwa la Sahara. Akiwa mjini Niamey Guterres aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kutambua kuwa madhila ya Niger siyo ya kikanda au bara la Afrika pekee bali ni kitisho kwa ulimwengu mzima.

Kwa kuitembelea Nigeria hapo jana, Guterres amekamilisha ziara yake katika mataifa matatu ya Afrika Magharibi iliyoanzia nchini Senegal mwishoni mwa juma lililopita.