1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aitolea mwito Urusi kumaliza vita Ukraine

23 Machi 2022

Maelfu ya raia wa Ukraine wanajaribu kuukimbia mji wa Mariupol wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ya mabomu kwenye mji huo wa bandari.

Ukraine-Konflikt - UN-Sicherheitsrat
Picha: Richard Drew/AP/dpa/picture alliance

Maelfu ya raia wa Ukraine wanajaribu kuukimbia mji wa Mariupol wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ya mabomu kwenye mji huo wa bandari.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameitolea mwito Urusi kumaliza vita hivyo. Guterres amesema vita hivyo havina maana. Kulingana na shirika la Human Rights Watch, watu waliofanikiwa kuukimbia mji huo wameelezea hali mbaya walioiacha ikiwemo maiti kutapakaa barabarani na majengo yaliyoharibiwa.

Soma pia:Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine

Ukraine yasema mji wa Mariupol umegeuka uwanja wa mapambano

Hii ndio hali ilivyo katika mji wa MariupolPicha: Nikolai Trishin/ITAR-TASS/IMAGO

Baraza la mji wa Mariupol limesema mashambulizi ya anga ya Urusi yanaugeuza mji huo kuwa majivu, huku Marekani na washirika wake wa Ulaya wakipanga vikwazo zaidi ili kuiadhibu Urusi kwa uvamizi wake nchini Ukraine.

Maafisa wa Ukraine wamesema mapigano na mashambulizi ya mabomu yamechacha mjini Mariupol, siku moja baada ya kukaidi agizo la Urusi la kuwataka wanajeshi wa Ukraine kuweka chini silaha na kusalimu amri.

Maelfu ya watu wanaaminika kukwama ndani ya majumba, bila ya chakula, umeme, maji na mahitaji mengine ya msingi.

Shirika la habari la Urusi-RIA limeripoti kwa kumnukuu kiongozi wa wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Urusi kwamba vikosi vya usalama vya Urusi na wapiganaji hao wamedhibiti karibu nusu ya mji wa bandari ya Mariupol, ambao ni nyumbani kwa watu wapatao 400,000.

Wakaazi wa Mariupol wamekosa huduma muhimu za msingi

Raia wa Ukraine wakijaribu kuukimbia mji wa MariupolPicha: Bernat Armangue/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa gavana wa jimbo la Mariupol, mapigano makali yameripotiwa katika mji huo wa bandari, huku raia na wanajeshi wa Ukraine wakishambuliwa kwa risasi na vikosi vya usalama vya Urusi. Naibu meya wa Mariupol Sergei Orlov ameliambia shirika la habari la Marekani CNN kuwa, mji huo umezingirwa na kwamba hawajapokea msaada wowote wa kibinadamu. Katika ujumbe wa video alioutoa wakati akilihutubia bunge la Italia, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy amesema na, "Hakuna kitu kilichosalia hapa. Tutawezaje kufanya kilimo wakati tunashambuliwa na silaha za Urusi?" 

Soma pia: Ukraine yajaribu kuwasajili wapiganaji wa kiafrika

Zelensky amesema mazungumzo na Urusi yakumaliza vita hivyo ni magumu na wakati mwengine yenye cheche kali, japo ameongeza kuwa hatua kwa hatua wanafanya kila wawezalo kuhakikisha mazungumzo hayo yanazaa matunda.

Licha ya wawakilishi kutoka pande zote kukaa kwenye meza ya mazungumzo, pande zote mbili zimesema safari ya kupatikana mwafaka bado ni ndefu. Mji wa Mariupol umekuwa ukilengwa na wanajeshi wa Urusi kutokana na umuhimu wake kijografia. Mji huo uko katika bahari ya Azov na kuchukuliwa kwake kutairuhusu Urusi kuunganisha maeneo ya mashariki yanayodhibitiwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga na Ukraine, na wanaoungwa mkono na Urusi.

Biden kufanya ziara Brussels kujadili juu ya vita vya Ukraine

Rais Joe Biden wa Marekani Picha: dam Schultz/White House/Planet Pix/picture alliance/ZUMAPRESS

Rais wa Marekani Joe Biden na washirika wake wa Ulaya wanatarajiwa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi pamoja na hatua mpya za kuimarisha vikwazo vilivyopo wakati wa ziara yake mjini Brussels wiki hii.

Katika ziara hiyo, Biden pia atajadili juu ya marekebisho ya muda mrefu ya muungano wa jeshi la kujihami NATO kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia. Rais huyo wa Marekani pia atatangaza hatua ya pamoja ya kuimarisha usalama wa nishati barani Ulaya, ambayo hutegemea sana gesi kutoka Urusi.

Biden ameahidi kutotuma wanajeshi wa Marekani nchini Ukraine, japo amesisitiza ahadi ya Washington ya kulinda wanachama wa NATO iwapo mmoja wao atashambuliwa. Rais huyo wa Marekani anaelekea Brussels leo Jumatano kwa ajili ya mkutano wa siku ya Alhamisi na viongozi wa Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW