1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Guterres aizuru Somalia

11 Aprili 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili mjini Mogadishu huko Somalia Jumanne kuanza ziara fupi katika nchi hiyo iliyozongwa na mapigano na majanga ya kimazingira.

Katar, Doha | UN LDC5 Konferenz
Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Alipowasili, Guterres amekaribishwa na waziri wa mambo ya nje wa Somalia Abshir Omar Huruse ambaye amechapisha picha za kuwasili kwake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari nchini Somalia, Guterres ambaye aliizuru Somalia mnamo mwezi Machi mwaka 2017, atafanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa nchini humo kisha baadae aitembelee kambi moja ya wakimbizi wa ndani.

Serikali ya Somalia imeufunga mji wa Mogadishu kwasababu ya ziara hiyo huku barabara nyingi zikiwa zimefungwa na usafiri wa umma ukiwa umepunguzwa pakubwa.

Pembe ya Afrika kukosa mvua kwa misimu mitano mfululizo

Ziara yake inafanyika wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na ukame mkubwa uliowasukuma wengi katika baa la njaa huku serikali ikiwa katika mapambano makali ya kutaka kuliangamiza kundi la kigaidi la al-Shabab.

Somalia, Kenya na Ethiopia zimejikuta zikikabiliana na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo la Pembe ya Afrika kwa kipindi cha miongo minne kutokana na kukosekana kwa mvua kwa misimu mitano mfululizo. Ukame huo umesababisha vifo vya mifugo na mazao na kuwapelekea angalau watu milioni 1.7 kuyahama makaazi yao kwa ajili ya kutafuta maji na chakula.

Wanawake wa Somalia walioathirika na ukame unaozidi nchini humoPicha: Feisal Omar/REUTERS

Huku ikiwa nchi ya Somalia haijafikia kiwango kinachoweza kusemekana kwamba ni uhaba mkubwa wa chakula, Umoja wa Mataifa unasema karibu nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo watahitaji misaada ya kiutu mwaka huu, huku ikiwa watu  milioni 8.3 wameathirika na ukame.

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa msaada wa kiutu wa dola bilioni 2.6 kwa Somalia ila umepokea asilimia kumi na tatu tu ya fedha hizo.

Ikiwa mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, kwa miongo kadhaa sasa Somalia imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. machafuko ya kisiasa na mashambulizi yanayofanywa na kundi la itikadi kali la Al-Shabab lililo na mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Maeneo kadhaa yakombolewa Somalia

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahmoud mwaka jana alitangaza "vita kamili"na wanamgambo wa kundi hilo na mnamo mwezi Septemba akatuma vikosi ili kutoa usaidizi kwa mashambulizi yaliyoanzishwa na wanamgambo wa kijiji kimoja katikati mwa Somalia dhidi ya Al-Shabab.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh MahmoudPicha: Abukar Mohamed Muhudin/AA/picture alliance

Katika miezi ya hivi majuzi, jeshi na wanamgambo hao wakiungwa mkono na kikosi cha Umoja wa Afrika, ATMIS, na mashambulizi ya angani ya Marekani, wamefanikiwa kunyakua maeneo kadhaa kupitia operesheni hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ripoti iliyoitolewa katika Baraza la Usalama mwezi Februari, alisema tangu mwaka 2017, mwaka 2022 ndio uliokuwa mwaka mbaya zaidi kwa Wasomalia kutokana na mashambulizi ya Al-Shabab.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW