1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Guterres alaani mauaji ya wafanyakazi wa UN Gaza

13 Septemba 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mauaji ya wafanyakazi sita ya shirika la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, katika mashambulizi ya Israel dhidi ya shule iliyogeuzwa hifadhi Gaza.

Kim Jong Un akitembelea taasisi ya silaha za nyuklia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.Picha: BEN MCKAY/AAP/IMAGO

Mashambulizi hayo ya Jumatano yalilenga shule inayohifadhi familia za Wapalestina waliopoteza makaazi yao pamoja na kaya mbili, na kuuwa dazeni kadhaa.

Guterres amesema katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa X kuwa ukiukaji huo wa sheria ya kimataifa unapaswa kukoma sasa.

Jeshi la Israel lilithibitisha mashambulizi hayo jana Alhamisi, likisema lilifanya shambulio la usahihi dhidi ya magaidi waliokuwa ndani ya kituo cha kamandi ya Hamas.

WHO yahamisha wagonjwa 97 kutoka Gaza

Wakati huo huo, shirika la afya duniani WHO, lisema kuwa limehamisha wagonjwa 97 nje ya Gaza, ikiwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa kuhamishwa tangu Oktoba 7.

Mwanamke wa Kipalestina akimkumbatia mwanae baada ya shambulizi la Israel dhidi ya shule ya al-Jaoun, Septemba 11, 2024.Picha: Moez Salhi/Anadolu/picture alliance

Wagonjwa waliohamishwa walikuwa wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali yakiwemo saratani, magonjwa ya damu na ini, na kiwewe, na karibu nusu yao walikuwa watoto.

Wagonjwa hao walihamishwa kwa njia ya barabara, na kisha kwa ndege kutoka uwanja wa ndege wa Ramon nchini Israel hadi Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya matibabu.

Soma pia: Israel yaua makumi baada ya kushambulia maeneo ya Palestina

Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisifu ufanisi wa operesheni hiyo aliyoitaja kuwa ngumu..licha ya changamoto kali za uendeshaji na ukosefu wa usalama.