1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Guterres alaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

23 Februari 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine akisema ni dharau, na kwamba kumbukumbu ya mwaka mmoja wa vita hivyo ni hatua mbaya kwa watu wa Ukraine na jumuia ya kimataifa.

Ukraine Bachmut | Ukrainische Panzer
Picha: Alex Babenko/REUTERS

Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza Kuu kilichofanyika Jumatano, Guterres amesema uvamizi huo unakiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa na amevikosoa vitisho vya Urusi kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia.

Wakati mapigano yakiendelea Ukraine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litafanya kikao maalum kujadili azimio linaloungwa mkono na Ukraine na washirika wake, ambalo linataka kuwepo kwa amani ya haki na ya kudumu, litakalopigiwa kura baadae Alhamisi, kuelekea mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 24.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Mary Altaffer/AP Photo/picture alliance

Ingawa hatua hizo sio ngumu kama ambavyo Ukraine inataka, kuna matumaini kwamba mataifa mengi ya Umoja wa Mataifa yataliunga mkono azimio hilo lisilo la kisheria la kuonesha kuwa Ukraine inaungwa mkono na jumuia ya kimataifa. Azimio hilo pia linataka kusitishwa kwa uhasama, na Urusi kuyaondoa majeshi yake mara moja nchini Ukraine bila kutoa masharti yoyote yale.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya amezishutumu nchi za Magharibi kwa kujiandaa kuitoa muhanga Ukraine na ulimwengu ulioendelea ili kuishinda Urusi. Akizungumza katika kikao hicho maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Nebenzya amesema Marekani na washirika wake wa Ulaya wanapuuzia ''unazi mamboleo'' nchini Ukraine kwa kuitumia nchi hiyo kuisashambulia Urusi.

Nebenzya: Wanataka kuitumbukiza dunia vitani

''Sasa wanashindana wao kwa wao kuweka vikwazo kwenye nchi yangu. Ingawa vikwazo hivi kiukweli vinaziathiri zaidi nchi zinazoendelea. Kwa matamanio yao ya kuishinda Urusi kwa njia yoyote ile, hawawezi tu kuitoa Ukraine muhanga, wako tayari kuutumbukiza ulimwengu wote kwenye janga la vita,'' alisisitiza Nebenzya.

Aidha, Nebenzya ameishutumu Ujerumani na mataifa ya Magahribi kwa kuonesha nia ya kuuingilia mzozo wa Ukraine sawa na zile za Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Amesema vita vya Ukraine ni sawa na ilivyokuwa miaka 80 iliyopita, ambapo iliwahusisha maadui wasaliti na mataifa yenye nguvu ambayo yanataka kuichukua ardhi yao na kuwatisha.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin akilihutubia Bunge la Shirikisho la UrusiPicha: Sergei Karpukhin/TASS/IMAGO

Wakati huo huo, Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema nchi yake itadumisha umakini zaidi katika kuongeza nguvu zake za nyuklia. Kauli hiyo ameitoa Alhamisi siku moja kabla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu ilipoivamia Ukraine.

Putin amesema pia Rais wa China, Xi Jinping ataizuru Urusi, akisema uhusiano wao umefikia mipaka mipya. Marekani ina wasiwasi kuwa China inaweza kuipatia Urusi silaha za kivita katika vita vyake vya Ukraine.

Mke wa rais wa Ukraine azungumzia ukiukaji wa haki za binaadamu

Huku hayo yakijiria, Olena Zelenska mke wa rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameelezea kuhusu ukiukaji wa haki za binaadamu nchini humo kutokana na uvamizi wa Urusi. Akizungumza siku ya Jumatano katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, Zelenska amesema wana haki ya kuishi kwa uhuru na sio kuuawa au kuteswa.

Zelenska alionesha mkanda wa video katika eneo la mapambano la Bakhmut, mji ambao vikosi vya Urusi vinajaribu kuuteka, ambako mashambulizi yamewaua raia na kuharibu miundombinu ya kijamii.

Ama kwa upande mwingine, maafisa wa Ukraine wamesema raia wawili wameuawa kwa mashambulizi ya Urusi kwenye jimbo la Kherson kusini mwa Ukraine na wengine wawili wamejeruhiwa kwa shambulizi la kombora katika mji wa Kharkiv.

(AP, AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW