Guterres: Amerika kusini na karibiki ni kitovu cha COVID-19
10 Julai 2020Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres jana alipotoa ujumbe kwa njia ya vidio na kusema kunywea kwa pato jumla la taifa GDP kunatarajiwa mwaka huu katika eneo hilo, ambalo litakuwa kubwa zaidi katika kipindi cha karne moja.
"COVID-19 inawakilisha mshituko mkubwa wa kiafya, kijamii na kiuchumi utakaoambatana na matatizo makubwa ya kiutu katika nchi za Amerika ya kusini na visiwa vya Karibiki," ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema.
Hali hiyo inatarajiwa kusababisha mdororo mkubwa kabisa wa kiuchumi katika enzi hizi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa mataifa, ukosefu wa ajira katika kanda hiyo ya Amerika kusini unatarajiwa kupanda hadi asilimia 13.5 kutoka asilimia 8.1 mwaka jana, ukiathiri zaidi ya watu milioni 44, ikilinganishwa na zaidi ya watu milioni 18 mwaka 2019. Kiwango cha umasikini kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 37.2 kutoka asilimia 30.2, ikiwa na maana watu milioni 230 wataathirika ikilinganishwa na watu milioni 185 mwaka jana , taarifa hiyo imesema.
Hali mbaya Latin Amerika
Guterres alisema Amerika kusini na visiwa vya Karibiki tayari zinakabiliwa na, "hali mbaya ya kutokuwa na usawa," viwango vya juu vya ajira ambazo si rasmi na huduma mbovu za afya, na watu ambao wamo katika hatari kubwa katika kanda hiyo" kwa mara nyingine tena wanaathirika kwa kiwango kikubwa " na COVID-19
"Wanawake, wazee, watu wenye ulemavu, jamii ya watu wa asili, watu wenye asili ya Afrika, pamoja na wahamiaji na wakimbizi," pia wanateseka kwa kiwango kikubwa, wakati hali mbaya ikiongezeka."
Wakati huo huo zaidi ya kesi 60,500 za maambukizi mapya zimeripotiwa nchini Marekani hadi jana, kwa mujibu wa hesabu iliyowekwa pamoja na shirika la habari la Reuters, ikiwa weka rekodi ya maambukizi ya siku moja wakati Wamarekani wenye hofu wakiambiwa wachukue tahadhari zaidi na janga hilo litumiwa kisiasa zaidi.
Nchini Ujerumani idadi ya kesi za maambukizi zilizothibitishwa zimeongezeka kwa watu 395 hadi watu 198,178, data kutoka taasisi ya kuzuwia magonjwa ya Robert Koch zimeonesha leo.
Nae waziri wa uchumi wa Japan amesema leo kuwa hatua mpya zinahitajika kuzuwia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona katika vilabu vya usiku na mabaa, ambavyo vimeonekana sasa kuwa ni chanzo cha maambukizi.