Guterres ana matumaini ya kupatikana suluhu Korea
3 Mei 2018Katika mahojiano maalumu na BBC Radio 4 jijini London nchini Uingereza, Guterres amesema anaamini mambo yanakwenda katika mkondo ulio sahihi kuelekea mazungumzo ya maana yatakayoleta tija. Amesema ni kwa masilahi ya raia wa Korea Kaskazini ambao wameathiriwa kwa kiwango kikubwa na vikwazo, ni masilahi ya Korea Kusini inayohitaji amani na usalama na ni kwa masilahi ya China ambayo muda wote imekuwa ikipinga Korea Kaskazini inayomilika silaha za nyuklia, lakini pia wakati huo huo ikitaka pawepo na mfumo imara wa usalama katika eneo hilo.
Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema kwamba jitihada zinazoshuhudiwa hivi sasa katika rasi ya Korea pia ni kwa maslahi ya Mareakni kwa sababu muda wote suala la kuhakikisha eneo la Korea halina silaha za nyuklia, limekuwa lengo kuu la utawala wa mjini Washington.
Awali Guterres alikutana na waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, ambapo walizungumzia masuala kadha wa kadha likiwemo kushirikiana kwa karibu zaidi kurejesha tena utaratibu wa sheria za kimataifa dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia na silaha za sumu.
Guterres alisema, "Tunafuatilia kwa karibu sana kuhakikisha kwamba nchi zote ulimwenguni zinaheshimu sheria na utaratibu uliopo na tumepania kufanya kazi kuhakikisha tunarejesha hali kuwa shwari mahala popote palipo na tatizo. Nadhani tunakabiliwa na suala zito la kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia na silaha za sumu. Hili ni mojawapo ya masuala yanayotutia wasiwasi na tutafanya kazi kwa bidii. Nafikiri kuhusu suala la nyuklia yapo matumaini, lakini suala la silaha za sumu bado safari ni ndefu."
China yaikaribia Korea Kaskazini
Wakati haya yakiarifiwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa China, Wang Yi, amekutakana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, wakati wa ziara isiyo ya kawaida mjini Pyongyang. Hayo yameripotiwa na wizara ya mambo ya kigeni ya China katika ukurusa wake rasmi kwenye mtandao wa kijamii. Wang amesema China itaendelea kuwa na jukumu muhimu katika kutafuta suluhisho la kisiasa katika rasi ya Korea, huku juhudi za kidiplomasia zikishika kasi katika eneo hilo.
Ziara hiyo ya siku mbili ya Wang Yi, afisa wa cheo cha juu kabisa wa China kufanya ziara nchini Korea Kaskazini katika kipindi cha miaka kadhaa, inafuatia mkutano wa kihistoria kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini na imefanyika kabla mkutano unaopangwa kati ya Kim Jong Un na rais wa Marekani, Donald Trump, katika wiki chache zijazo.
Kwa upande mwingine rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, ameutaka Umoja wa Mataifa kuhakiki mipango ya kufungwa kinu cha nyuklia cha Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa msemaji wa umoja huo, Moon amewasilisha ombi hilo kwa njia ya simu kwa katibu mkuu, Antonio Guterres, siku ya Jumatatu, siku chache baada ya Kim Jong Un kumwambia Moon Jae-in kwamba anapanga kukifunga kinu hicho mwezi huu wa Mei.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman