Guterres aonya kuhusu mwelekeo hatari wa vita nchini Ukraine
29 Mei 2026
Guterres ameliambia baraza la usalama kwamba "mashambulizi makubwa yaliyoanzishwa na Urusi kote nchini Ukraine katika siku za hivi karibuni yanaonyesha uzito na hali ya hatari kwa wakati huu."
Amesema kuwa hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota kwa kasi, na kurejea taarifa za Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, ambazo zinaonyesha kuwa tangu uvamizi wa Urusi kuanza Februari 2022, zaidi ya raia 15,000 wameuawa nchini Ukraine – wakiwemo watoto 800.
Aidha, ripoti kutoka Urusi zinaonyesha ongezeko la vifo vya raia ndani ya maeneo yanayodhibitiwa na nchi hiyo, vikiwemo vifo vya watoto.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za dharura za kupunguza uhasama, akitoa mwito wa "usitishaji kamili na usio na masharti wa mapigano mara moja.” Amesisitiza kuwa njia pekee ya kuzuia madhara zaidi ni kurejesha mazungumzo ya kidiplomasia na kuhakikisha kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu zinaheshimiwa na pande zote.