1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aonya kuhusu ongezeko la joto duniani

3 Desemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameikosoa jamii kwa kushindwa kupambana na ongezeko la joto duniani na amesema uongozi wa Marekani ni muhimu katika kushughulikia dharura ya mabadiliko ya tabianchi.

BdTD Australien Sturmwolken über Sydney
Picha: Getty Images/AFP/P. Parks

Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Chuo Kikuu cha Colombia, mjini New York, Marekani, Guterres ameonya kuwa hali ya sayari imevunjika na ubinadamu unasababisha vita vya asili.

Amesema viwango vya joto kali, ukame pamoja na bahari kufikia rekodi za juu za joto zinasababishwa na utunzaji mbaya wa mazingira unaofanywa na mwanadamu, na ametoa wito wa kutokuweko kwa gesi chafu ya kaboni. Amesema mapambano ya janga la mabadiliko ya tabianchi ni kipaumbele cha juu katika karne ya 21.

''Tunalazimika kuchukua haraka hatua tatu muhimu katika kuushughulikia mzozo wa hali ya hewa. Kwanza, tunahitaji kutokuwa na gesi chafu ya kaboni ndani ya miongo mitatu ijayo. Pili, tunapaswa kuweka sawa fedha za kimataifa nyuma ya Mkataba wa Paris, mwongozo wa ulimwengu wa hatua za kuchukua kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Na tatu, lazima tufanikiwe kuilinda dunia na hasa watu na nchi zilizoko katika hatari zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,'' alisisitiza Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres Picha: Manuel Elías/UN Photo/Imago Images

Akizungumzia kitisho kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa hakuna njia ya kulishughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi bila uongozi wa Marekani.

Mchango wa Marekani na China

Amesema makubaliano ya kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi yasingeweza kufanikiwa bila ushirikiano wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, akisema kuwa mkutano wa kilele kati ya Obama na Rais wa China, Xi Jinping ulisaidia kupatikana kwa uungwaji mkono wa China.

Soma zaidi: Trump aiondoa Marekani mkataba wa Tabianchi

Kuhusu ripoti ya awali ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO kuhusu hali ya mabadiliko ya tabianchi Ulimwenguni mwaka 2020, ambayo ilizinduliwa siku ya Jumatano, Guterres amerudia kusema kuwa muongo uliopita ulikuwa na rekodi ya juu ya joto na kwamba barafu ilipungua, majanga ya moto na vimbuga ambavyo havijawahi kutokea, zilikuwa tu baadhi ya athari.

Moto ukiwaka katika maeneo ya SiberiaPicha: Copernicus Sentinel/Sentinel Hub/Pierre Markuse

Kulingana na ripoti hiyo, mwaka 2020 huenda ukawa moja kati ya miaka mitatu iliyokuwa na joto kali zaidi duniani tangu kuanza kurekodiwa kwa viwango vya juu vya joto katikati ya karne ya 19.

Amewataka watu kuacha kukata miti ambako kunachangia mabadiliko ya tabianchi na kuanza kuiponya dunia kwa kupatana nayo. Guterres amesema sera za mabadiliko ya tabianchi zimeshindwa kuifikia changamoto hiyo, akibainisha kuwa utoaji wa gesi chafu kwa mwaka 2020 ulikuwa asilimia 60 zaidi kuliko mwaka 1990.

Amesema dunia inaelekea kwenye ongezeko la joto kwa kiasi cha nyuzi joto 3 hadi 5 za Celsius ifikapo mwaka 2100. Mwaka 2019 pia ulishuhudia kiwango cha juu zaidi cha joto la maji ya baharini.

(DPA. AFP, Reuters, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW