Guterres: Amani haiji Gaza mpaka vita visimame
24 Septemba 2025
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza juu ya amani ya kudumu huko Gaza amesema kulifikia lengo hilo inahitaji kujitolea kwa pamoja katika ngazi za kidiplomasia, kufuata sheria za kimataifa na kuheshimu utu wa watu wote.
Hata hivyo Vikosi vya Israel vinaendelea kufanya mashambulizi Gaza. Msemaji wa ulinzi wa raia katika eneo hilo amesema Wapalestina 15 wameuawa wakati majeshi ya Israel yaliposhambulia nyumba na mahema katika mji wa Gaza City.
Viongozi mbalimbali katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wameelezea masikitiko na kutoa mapendekezo juu ya kuvimaliza vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump kweli anataka sana kushinda tuzo ya amani ya Nobel, basi anahitaji kuhakikisha vita huko Gaza, vimesimamishwa kwa sababu ni yeye pekee ndiye ana uwezo wa kuishinikiza Israel ivimalize vita hivyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba serikali ya Israel imesababisha hali mbaya ya kibinadamu kwa kuendeleza mashambulizi makubwa kwenye mji wa Gaza City. Cooper amesema hatua ya Israel itafanya iwe vigumu kuwakomboa mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.
Marekani siku ya Jumanne ililikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kwamba nchi kadhaa kuu za Magharibi hivi karibuni zimeitambua Palestina kuwa ni taifa huru.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz, ameutaja mkutano wa Umoja wa Mataifa ulioitishwa na Ufaransa na Saudi Arabia siku ya Jumatatu kuwa, ulikuwa ni wa kiutendaji tu. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya kuhimiza kupatikana suluhisho la serikali mbili moja ya Waisrael na nyingine ya Wapalestina.
Mengineyo ni pamoja na taarifa kutoka kwa waandaaji wa msururu wa boti zilizobeba misaada na wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina zinazoelekea Gaza wamesema milipuko ilisikika na ndege zisizo na rubani zililenga baadhi ya boti zao, ambazo kwa sasa ziko karibu na Ugiriki.
Kundi hilo limesema hakuna aliyejeruhiwa. Flotilla ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za mashirika ya kiraia za kupinga vikwazo vya baharini kuelekea Gaza. Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, waandaaji hao wametoa wito wa hali inayowakabili kuzingatiwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Vyanzo: DPA/AFP