1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matembezi ya dharura ya Guterres nchini Somalia

Najma Hamis8 Machi 2017

Katiku Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameihimiza Jumuiya ya Kimataifa ichukue hatua ili kuepusha balaa la njaa nchini Somalia ambapo hali mbaya ya ukame imewaacha watu milioni tatu kukabiliwa na njaa.

Somalia Mogadischu - U.N. Generalsekretär Antonio Guterres bei Pressekonferenz
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Reuters/F. Omar

Somalia inakabiliwa na janga kubwa la njaa,hii ikiwa ni mara ya tatu nchi hiyo kujikuta katika baa la njaa miaka 25 tangu kuwepo kwa  vita vya wenyewe kwa wenyewe na machafuko ya kisiasa nchini humo. Mwaka 2011 watu 260,000  walikufa nchi humo kutokana na baa la njaa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa ziarani nchini Somalia alikuwa na ujumbe huu kwa jumuiya ya Kimataifa.

"Kuna uwezekano wa kuepukana na matatizo zaidi. Kuna nafasi na kuepukana na kile kilichotokea Somali mwaka 2011. Kuna ushirikiano mzuri baina ya rais, serikali na jumuiya ya kibinadamu, Jamii ya umojaa wa mataifa, msalaba mwekundu na hilali nyekundu. Kuna mpango wakufanya kitu.Upo uwezo lakini tunahitaji uungaji mkono mkubwa kutoka Jumuiya ya Kimataifa ili kuepusha marudio ya janga kubwa lililotokea mwaka 2011,'' alisema Guterres.

Guterres aliingia mjini Mogadishu katika ziara ya harakaharaka itakayomfikisha pia  katika kambi ya wakimbizi wa ndani katika sehemu zilizoathirika sana nchini humo.

Ama kwa upande mwingine Rais Mohamed Abdulllahi Mohamed,ambaye pia amekutana kwa mazungumzo na katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa  amesisitiza kilio chake kuhusu kuchukuliwa hatua za haraka kuiepusha nchi yake kutumbukia katika janga kubwa la maafa yanayosababishwa na njaa.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi FarmajoPicha: REUTERS/F. Omar

"Sababu ya kuwepo  kwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchi Somalia ni kuunga mkono na kuonesha ushirikianao kwa  watu wa Somali katika hali hii ngumu ya mgogoro huu wa kibinadamu,” alisema Raisi Farmajo wa Somalia. "Tunaathiriwa na ukame ambao unaweza kuwa janga la njaa, kama hatutopata mvua katika miezi miwili ijayo,”  aliongezea rais huyo.

Nchi nyengine za Afrika pia zinakubwa na njaa

Raisi huyo pia alionya kuwa hakutokuwa na mabadiliko ya haraka nchini Somali kama wanavotarajia wasomali.Kadhalika amesema matatizo ya Somali ni migogoro na ukame wa miaka 20, kwahiyo suluhisho pia litachukua zaidi ya miaka ishirini.

Umoja wa Mataifa umesema mwezi uliopita kwamba  dola bilioni 4.4 zinahitajika haraka  kushughulikia mgogoro huu katika nchi nne, ambapo watu zaidi ya milioni 20 wanakabiliwa na njaa.

Sudan Kusini, watu 100,000 tayari wanateseka na  janga la njaa "lililosababishwa na watu" kutokana na miaka mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Nchini Somalia, ukame umesababisha kuenea kwa magojwa ya kuharisha, kipindupindu na shurua, na watu karibu milioni 5.5 wako katika hatari ya kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

Hali ya kiangazi iliyosababishwa na ukosefu wa mvua imeathiri vibaya sana pia mataifa mengine ya Afrika ya Mashariki kama vile Ethiopia, Kenya na  mengi ya Kusini mwa Afrika.

Mwandishi: Najma Said

Mhariri: Saumu Yusuf