Guterres atoa rai ya mshikamano "kuunusuru ulimwengu"
14 Septemba 2022Kupitia hotuba yake aloitoa usiku wa kuamkia leo (14.09.2022) kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Guterres amesema dunia inakabiliwa na changamoto lukuki zinazohitaji mshikamano miongoni mwa mataifa duniani kuzitafutia majibu.
Amesema vizingiti hivyo ikiwemo Mabadiliko ya Tabianchi, umasikini, ukosefu mkubwa wa chakula na migawanyiko ni "kitisho" kwa juhudi za kufikiwa amani ya kudumu, haki za binadamu na maendeleo endelevu duniani.
Hotuba hiyo ya Guterres ambayo ndiyo inafungua rasmi mkutano wa ngazi ya juu wa kila mwaka wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa imeanisha umuhimu wa mataifa kushirikiana na kudhihirisha nafasi ya Umoja huo katika kuzitatua changamoto za dunia.
"Ulimwengu unawatizamia wajumbe wa Baraza Kuu kutumia zana zote tulizonazo kujadiliana, kupigia upatu mwafaka na suluhisho. Mkutano huu wa 77 unafaa kuwa muda wa mageuzi - kwa watu na sayari yetu pia. Muda ni sasa" amesema Guterres.
Guterres akumbusha wajibu wa kuonesha umuhimu wa mashirika ya kimataifa
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema bila kificho kwamba changamoto nyingi zilizougubika mkutano uliopita wa Baraza kuu la Umoja huu kwa sehemu kubwa bado hazijatatuliwa hadi sasa.
Amesema jukwaa la mwaka ndiyo sehemu sahihi ya kutafuta majibu. Amewakumbusha viongozi na wanadiplomasia wanaokwenda mjini New York kwa mkutano huo kwamba ni lazima watanabahi kuwa macho ya ulimwengu yanawatizama na mkutano huo utakuwa kipimo cha uthabiti wa asasi za kimataifa kwenye kutatua wa masuala mazito duniani.
Kwa upande wake rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa, Csaba Kőrösi, amewarai viongozi na wanadiplomasia watakaokwenda New York kukumbuka wajibu waliotwikwa na watu bilioni 8 duniani kutimiza matarajio yao.
Wiki inayokuja wakuu wa nchi na serikali kote duniani wataanza kumiminika mjini New York kuhutubia mbele ya Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.
Ingawa hakuna mabadiliko ya ratiba yaliyotangazwa, mazishi ya Malkia Elizabeth wa II yatakayofanyika wiki ijayo na ambayo viongozi wengi wa ulimwengu wanatarajiwa kushiriki huenda yataingilia kwa sehemu fulani ratiba ya mkutano wa Baraza Kuu.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema mkutano wa pembezoni wa masuala ya elimu uliopangwa Jumatatu ijayo na ambao viongozi wa nchi 90 wameahidi kushiriki utaendelea kama ulivyopangwa.
Urusi yaituhumu Marekani kwa "kukiuka wajibu wake" utoaji wa Viza
Ufunguzi wa mkutano wa mwaka huu umeanza kwa msuguano kati ya Marekani na Urusi baada ya Washington kutoa viza kwa wanadiplomasia wachache wa Urusi wanaopanga kwenda mjini New York.
Washington imetoa viza 24 pekee badala ya 56 zilizoombwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi. Miongoni mwa waliopatiwa viza ni waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov.
Hata hivyo Moscow imesema Marekani inakiuka wajibu wake chini ya mkataba wa kuundwa Umoja wa Mataifa, ambao unataka nchi mwenyeji wa makao makuu ya Umoja huo kutoa ruhusa kwa wanadiplomasia wote duniani kuingia bila vizuizi.