1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres atoa wito wa uchaguzi huru na wa haki Tanzania

George Njogopa27 Oktoba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteres, ametoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika na uchaguzi mkuu Tanzania kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu.

USA I New York I Der Generalsekretär der Vereinten Nationen Antonio Guterres
Picha: Mike Segar/Reuters

Kupitia msemaji wake, Guteres amesema "mchakato wa uchaguzi huu haupaswi kumwacha kando mdau yoyote na kwamba matumaini ya Umoja wa Mataifa ni kwamba utafanyika kwa amani na utulivu."

Wito wa Guteres unakuja wakati mandalizi ya uchaguzi huo yakiwa yamekamilika na kinachosubiriwa ni Oktoba 28 kwa wananchi kuanza kujitokeza katika vituo vya kupigia kura.

Katika tamko lake fupi, kuhusiana na uchaguzi wenyewe, Guteres amesema wale wote wenye fursa ya kuchagua na kuchaguliwa wanapaswa kupewa nafasi ya kutimiza matakwa yao ya kidemokrasia na kusisitiza wagombea ikiwamo wanawake wapewe kipaumbele.

Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Zanzibar Maalim Seif akamatwa

Amesema mamlaka zinazosimamia uchaguzi huu zinatimiza wajibu wake kwa kuweka mazingira ambayo yatatoa fursa kwa vyama vya siasa na wagombea wao kushiriki kikamilifu ili kulinda misingi ya amani iliyojengeka Tanzania kwa muda mrefu.

Katibu huyo mkuu amesema, Umoja wa Mataifa uko tayari kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha maendeleo endelevu na kujenga mustakabali mwema. Wakati Guteres akitoa wito huo, mashirika ya kiraia nchini Tanzania yamekuwa yakitoa ujumbe wenye kuhimiza mshikamano na kuzingatiwa kwa haki kwenye mchakato huo wa uchaguzi.

Matatizo ya Intaneti kabla ya uchaguzi

Ingawa baadhi ya mashirika hayo yameonya kuhusu kuzorota kwa uhuru wa maoni na vyombo vya habari, lakini Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umewataka wananchi kujitokeza kutimiza haki zao za kidemokrasia kwa kuwachagua viongozi waliowaridhia.

Mratibu wa (THRDC), Onesmo Olengurumwa mbali ya kutoa wito huo, pia amegusia kuhusu vyombo vinavyohusika na uchaguzi huo kuendesha majukumu yao kwa kuzingatia haki na wajibu wao.

Wafuasi wa chama cha upinzani Tanzania, CHADEMA, wakati wa kampeni za uchaguzi, Dar es SalaamPicha: DW/S. Khamis

 "Tunapenda kuvisihi vyombo vyote vinavyosimamia uchaguzi huo, viendelee kufanya majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kuisimamia haki ili uchaguzi uwe wa huru na haki," amesongeza Olengurumwa.

Katika hatua nyingine, serikali imewapa ruhusu watumishi wake walioko mbali na vituo walivyojiandikisha kupiga kura kurejea kwenye vituo hivyo ili kushiriki kwenye uchaguzi huo kesho.

Kwa mujibu wa waraka ulitolewa na serikali watumishi hao wameruhusiwa kuondoka kwenye maeneo yao ya kazi kuanzia Jumanne hapo Oktoba 29 watakapotakiwa kurejea kazini siku inayofuata.

Polisi Pemba yasema hali ni shwari

This browser does not support the audio element.

Kumekuwa na idadi kubwa ya watumishi wa umma waliobadilisha vituo vyao vya kazi hasa baada ya serikali kuanza kuteleza mpango wa kuhamishia makao makuu jijini Dodoma.

Wakati hayo yakiwa hivyo, siku moja kabla ya kuelekea uchaguzi wenyewe kumekuwa na tatizo la mawasiliano ya mtandao wa internet na wengi wanajikuta wakipata ugumu wa kupakua na kutuma picha kupitia mitandao yao.

Tatizo hilo limeanza kushuhudiwa tangu Jumanne  asubuhi ambako wengi wao wakijikuta wakishindwa kutumia huduma hizo kwa ufanisi kama ilivyokuwa siku zote.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW