1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Guterres atoa wito wa usitishwaji mapigano Gaza

25 Oktoba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza na ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi dhidi ya Gaza yanakiuka sheria ya kimataifa.

USA New York | UN-Sicherheitsrat | Debatte über Nahost | Antonio Guterres, Generelsekretär
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani (24.10.2023)Picha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Katika matamshi aliyoyatoa kwa Baraza la Usalama jana Jumanne, Guterres alikosoa ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa unaoshuhudiwa Gaza na amesema Wapalestina wamekabiliwa na ukaliaji wa miongo kadhaa, kabla kuongeza kwamba ni muhimu kutambua mashambulizi yaliyofanywa na Hamas hayakufanyika katika ombwe.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan amejibu kauli hiyo kwa kumtaka Guterres ajiuzulu, akimtuhumu kuelewa na kukubaliana na ugaidi pamoja na mauaji katika mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan Picha: Mike Segar/REUTERSS

Erdan aliandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter na akasema kauli za Guterres zina maana hafai kuuongoza Umoja wa Mataifa.

Matamshi ya Guterres pia yamemghadhabisha waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen ambaye amemnyoshea kidole cha lawama Guterres na kupaza sauti yake akielezea jinsi raia, wakiwamo watoto wadogo, walivyouliwa Oktoba 7.

Cohen alifuta mkutano uliokuwa umepangwa kati yake na Guterres baada ya malumbano hayo. Cohen aliandika akisema hatakutana na katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. "Baada ya Oktoba 7 hakuna mtazamo wenye uwiano. Hamas lazima iangamizwe kabisa katika uso wa dunia".

Vita vyaendelea huko Gaza 

Israel imeendeleza mashambulizi dhidi ya maeneo mbalimbali ya kundi la Hamas huku viongozi wa makundi matatu ya wanamgambo wa Hamas, Islamic Jihad na Hezbollah tawi la Lebanon wakikutana. Miito ya usitishwaji mapigano imeendelea kutolewa hata na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress.

Raia wa Palestina wakijaribu kumuokoa mtoto kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya Israel huko Gaza (10.10.2023).Picha: Fatima Shbair/AP/picture alliance

Wizara ya Afya ya Palestina imesema leo hii kwamba tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas, zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel. Hata hivyo ghasia zilikuwa tayari zimeshamiri katika Ukingo huo hata kabla ya mzozo huu ulioibuka Oktoba 7,  huku kukiwa na idadi kubwa zaidi ya vifo huko Palestina ambayo ilikuwa haijashuhudiwa angalau tangu mwaka 2005.

Jeshi la Israel  limesema limezima jaribio la wapiganaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza waliojaribu kujipenyeza na kuingia Israel kupitia baharini. Milio kadhaa ya risasi ilisikika na wanamgambo kadhaa wameuwawa.

Mkutano wa Hamas, Islamic Jihad na Hezbollah 

Kiongozi Mkuu wa kundi la Hezbollah la huko Lebanon amekutana na viongozi wakuu wa makundi ya wapiganaji wa Palestina wa Hamas na Islamic Jihad, ili kujadili hatua ambazo muungano wao unaweza kuzichukua ili kupata "ushindi wa kweli."

Wanajeshi wa Israel wakiwasili katika eneo kaskazini katika mpaka wa Israel na Lebanon ambako kumekuwa kukishuhudiwa mapigano na kundi la Hezbollah. (18.10.2023) Picha: Ayal Margolin/JINI/Xinhua/picture alliance

Mkutano huo ambao haukutajwa ni lini na wapi ulipofanyika, uliwakutanisha Sayyed Hassan Nasrallah wa Hezbollah, Naibu mkuu wa Hamas Saleh al-Arouri na kiongozi wa Islamic Jihad Ziad al-Nakhala.

Kundi la Hezbollah  linalomiliki silaha nyingi na ambalo linaungwa mkono na Iran limekuwa likipambana na wanajeshi wa Tel Aviv kwenye mpaka wa Israel na Lebanon tangu vita vilipozuka kati yao na Hamas mnamo Oktoba 7.

Juhudi za usuluhishi katika mzozo huo

Rais Abdel Fattah al-Sisi amesema hii leo kuwa Misri inatumia vyema nafasi yake katika kujaribu kupunguza mzozo huko Gaza huku akisisitiza kutegemea zaidi suluhisho la kidiplomasia katika mzozo wa Palestina.

Naye Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, amerejelea leo Jumatano wito wake wa kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Wanamgambo wa Hamas huku akitoa pia wito wa kuruhusiwa  misaada ya kibinadamu kuwasilishwa kwenye Ukanda wa Gaza.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Gregorio Borgia/AP/picture alliance

Papa Francis amesema pia kwamba ataongoza sala maalum kwa ajili ya amani siku ya Ijumaa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, katika kile alichosema itakuwa ni "siku ya mfungo, sala na toba".

Soma pia: Israel yazidisha mashambulizi ya mabomu dhidi ya Gaza

Jared Kushner, ambaye alishiriki katika mazunguzo ya kufikia makubaliano ya amani kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu, amesema leo hii kwamba "Makubaliano ya Abraham" yana umuhimu zaidi kwa sasa kuliko hapo awali ukizingatia mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

Kushner ambaye alikuwa pia mshauri wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, amesema Israel inapaswa kuwa na usalama wake lakini Wapalestina hawana budi kuwa na fursa ya kuishi maisha bora.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW