Guterres autetea uteuzi wake wa mjumbe mpya wa Libya
12 Februari 2017Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema nchi yake haiungi mkono uteuzi huo kwasababu Mamlaka ya Palestina bado haina uanachama kamili katika Umoja huo. Haley pia alieleza sababu nyingine ni kuwa, kwa muda mrefu Umoja wa Mataifa umekuwa unaibagua Israel ambayo ni mshirika mkubwa wa Marekani na kuipendelea Palestina.
Hata hivyo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameeleza kwamba maafisa wa Umoja huo wanafanya kazi zao kuambatana na majukumu waliyopewa na wala hawaiwakilishi serikali au nchi yoyote.
Dujarric amesema uteuzi huo wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa umetokana na uwezo wa bwana Fayyad wa kuifanya kazi hiyo na kwamba Waisrael au Wapalestina hawajawahi kushikilia nyadhifa za juu kwenye Umoja wa Mataifa hali ambayo katibu mkuu Antonio Guterres anaonelea inapaswa kubadilika.
Wapalestina walipewa hadhi ya kuwa waangalizi katika Umoja wa mataifa mnamo mwaka 2012. Guterres anatafuta kuungwa mkono na wanachama wote 15 ili kukamilisha uteuzi wake wa Fayyad.
Ufaransa na Sweden zinaunga mkono uteuzi wa Fayyad. Bwana Fayyad mwenye umri wa miaka 64 aliwahi kuitumikia benki ya dunia na pia alikuwa waziri mkuu wa Mamlaka ya Palestina kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2013.Vile vile alikuwa ni waziri wa fedha wa Mamlaka ya Palestina. Wakati wa uongozi wake alisifiwa kwa kuendesha vita dhidi ya ufisadi na juhudi alizofanya katika kuzijenga taasisi za umma.
Uamuzi wa Marekani wa kuzuia uteuzi wa Fayyad umemshangaza katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, huu ukiwa ni uteuzi wake wa kwanza tangu achukue wadhifa huo kutoka kwa Ban Ki-Moon tarehe 1 mwezi Januari kwamba alichokuwa anakitarajia kuwa uteuzi wake utakubalika moja kwa moja na wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hakitawezekana.
Mjumbe wa kamati kuu ya chama cha ukombozi cha Palestina PLO Hannan Ashrawi ameilaumu Marekani kwa kuzuia uteuzi huo. Ashrawi amesema kwamba Marekani inafanya ubaguzi wa wazi. Salam Fayyad alipangiwa kuchukua mahala pa Martin Kobler kutoka Ujerumani ambaye amekuwa anashikilia wadhfa huo wa mjumbe maalum wa Libya tangu mwaka 2015.
Rais wa Marekani Donald Trump na balozi wake kwenye Umoja wa mataifa Nikki Haley wameulaumu Umoja wa Mataifa kwa azimio la mwezi Desemba mwaka uliopita lililoitaka Israel kusimamisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.
Balozi wa Israel katika Umoja wa mataifa Danny anon ameipongeza hatua ya Marekani na kuitaja kuwa ni mwanzo mpya ambapo Marekani inasimama kidete dhidi ya hatua zozote zinazolenga kuikandamiza Israel.
Jumatano wiki ijayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaujadili mzozo kati ya Israel na Palestina na siku hiyo hiyo,Rais Trump atakutana na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Mwandishi Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Caro Robi