1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres awakosoa walinda usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

17 Juni 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres avikosoa vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kile alichokitaja kuwa kuongezeka kwa vitisho na mashambulizi dhidi ya walinda amani na ukiukwaji wa haki. 

Konflikt in Nahost | Waffenruhe zwischen Israel und Gaza
Picha: Evan Schneider/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Ripoti ya Guterres ya kurasa 37 kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo shirika la habari la Associated Press limepata nakala yake, imesema watu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaendelea kukabiliwa na viwango vya juu na visivyokubalika vya machafuko.

Guterres alisema hali ya usalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati inasalia kuwa tete haswa upande wa magharibi, kaskazini magharibi na eneo la kati la nchi hiyo kufuatia muendelezo wa machafuko kati ya makundi yenye silaha, hali inayosababisha mauaji.

Soma pia: Uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakabiliwa na vurugu

Ametoa wito kwa Rais Faustin Archange Touadera kuyapa masuala ya amani na maridhiano kipaumbele katika muhula wake wa pili madarakani na atumie nafasi hiyo kushughulikia mizizi ya machafuko.

Wanajeshi wa kikosi cha mpakani katika Jamhuri ya Kidemokrasia Afrika ya Kati baada ya kupewa medali za kijeshi na Waziri Mkuu Firmin Ngrebada eneo la Boali Januari 10, 2021.Picha: Florent Vergnes/AFP/Getty Images

Machafuko ya mpakani na Chad Mei 30

Ripoti hiyo pia iliainisha machafuko yaliyotokea Mei 30 katika mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad na kuzidisha taharuki kati ya nchi hizo.  

Katika kipindi ambacho ripoti hiyo iliangazia, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSMA ulirekodi matukio 344 ya ukiukaji wa haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kiutu. Matukio hayo yaliathiri watu 628 na kusababisha vifo 82 kutokana na machafuko.

Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini limekumbwa na mapigano mabaya ya kijami na kidini tangu mwaka 2013.

Makubaliano ya amani baina ya serikali na makundi 14 ya waasi yalisainiwa Februari mwaka 2019. Lakini machafuko hayo yanayodaiwa kusababishwa na rais wa zamani Fracois Bozize bado yanaendelea huku washirika wake wakitishia kuuvunja mkataba huo wa amani.

Baadhi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mahakama yamzuia Bozize kuwania urais

Machafuko yalizuka baada ya mahakama ya kikatiba kumzuia Bozize kuwania urais Disemba mwaka uliopita.

Touadera alishinda uchaguzi huo kwa muhula wake wa pili kwa kupata asilimia 53 ya kura zote zilizopigwa. Lakini aliendelea kukumbwa na upinzani kutoka kwa vikosi vinavyohusishwa na Bozize.

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilishutumu vikali ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa kuhusu ubinadamu nchini humo na kuonya kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa mataifa nchini humo yanaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois BozizePicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Marekani na Urusi zanyosheana vidole vya lawama

Katika mkutano huo tete wa baraza la usalama, mratibu wa masuala ya kisiasa wa Marekani Rodney Hunter alielezea kusikitishwa kwake na ripoti kwamba maafisa wa kijeshi wa Urusi waliongoza vikosi vyao kufanya mashambulizi nchini humo. Ikiwa ni pamoja na makabiliano na walinda amani wa Umoja wa Mataifa, vitisho dhidi ya maafisa wa umoja huo, ukiukaji wa sheria ya kimataifa kuhusu misaada na huduma za kiutu, ubakaji, uporaji hata dhidi ya mashirika ya kutoa misaada.

Hata hivyo, naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Anna Evstigneeva, aliishutumu Marekani kwa kile alichokitaja kuwa madai yasiyokuwa na msingi na kwamba madai hayo ya Marekani na kampeni yake katika mitandao ya kijamii zinaashiria mpango wake- unaolenga kuharibu msaada wao imara wa kurejesha utulivu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

(AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW