1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres azindua kampeni kabambe ya utunzaji wa mazingira

Daniel Gakuba
13 Mei 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezindua kampeni kabambe ya kuhimiza hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, yanayoelezewa kuwa suala muhimu kabisa kwa wakati huu kuhusu mustakabali wa dunia.

Neuseeland Auckland Antonio Guterres und Jacinda Ardern
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kushoto) na Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern mjini AucklandPicha: Getty Images/H. Peters

Ziara hiyo ya Katibu Mkuu Guterres iliyoanzia New Zealand itamfikisha pia katika visiwa vingine kadhaa vya Kusini mwa Bahari ya Pasifiki, vikiwemo Fiji, Tuvalu na Vanuatu, ambavyo vimetajwa kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kupanda kwa kina cha bahari kunakokwenda sambamba na kuongezeka kwa joto duniani kunatishia kuvizamisha visiwa hivyo na kuyaweka hatarini maisha ya wakazi wake.

Soma zaidi: Utafiti: Mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho kikubwa duniani 

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern, Guterres ameisifu New Zealand kwa sera zake rafiki kwa mazingira, akaonya lakini kwamba ari ya kisiasa kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, imekuwa ikipungua. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewatolea mwito vijana kuongoza mipango ya kuyalinda mazingira ya dunia, akisema nchi zilizo na viongozi wenye umri mdogo zimekuwa zikiongoza utekelezwaji wa sera za kuzuia uchafuzi wa mazingira ya dunia.

Apinga matumizi ya kodi kwa ruzuku ya nishati chafu

Kwa hali ya kipekee, Guterres amezitaka serikali za nchi kuacha kutumia fedha za walipa kodi kudhamini shughuli za kiuchumi ambazo zinalaumiwa kuiweka dunia katika hatari iliyopo.

Wakazi wa visiwa vidogo wanatishiwa na kina cha bahari kinachozidi kupandaPicha: Getty Images/J. Aznar

''Ni ujumbe ulio wazi kwa serikali, kwamba ni muhimu kabisa kuacha kutumia fedha za walipa-kodi kutoa ruzuku kwa matumizi ya nishati chafu. Hilo ni kutumia pesa za walipa-kodi kuongeza vimbunga, kueneza ukame, mawimbi ya joto kali, kuangamiza matumbawe na kuharakisha kuyeyuka kwa theluji.'' Amesema Guterres na kuongeza kwamba fedha za walipa-kodi zinapaswa kuwekezwa katika maeneo yenye manufaa kwa ubinadamu.

 

Soma zaidi: Mswada wa mwisho wa mabadiliko ya tabia nchi kuwasilishwa

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern ameunga mkono mtazamo wa Guterres, akisema litakuwa jambo la hatari kabisa kupuuza tatizo la mabadiliko ya tabia-nchi, alilotaja kama changamoto nambari moja inayoikabili dunia.

Visiwa vidogo kuifungulia mashtaka Australia

Hayo yakijiri, kundi la visiwa vidogo vilivyo karibu na Australia vinatarajiwa kufikisha mashtaka katika Umoja wa Mataifa, dhidi ya mipango hafifu ya nchi hiyo katika kutunza mazingira ya dunia, hali ambayo visiwa hivyo vya Torres Straight vinasema inaweka hatarini maisha ya wakazi wake.

Kauli za Guterres na Adern zimetolewa wakati utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ukiwa umeiondoa nchi hiyo kubwa katika mkataba wa Paris wa kutunza mazingira. Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la kushughulikia mizozo -Richard Gowan, amesema hatua hiyo ya Trump imeiacha China ikionekana kuchukua jukumu la mdhamini mkuu wa mkataba wa Paris.

Kampeni hii ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na katibu wake mkuu, ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kilele kuhusu utunzaji wa mazingira ya dunia utakaofanyika  mjini New York badaye mwaka huu. Guterres amewataka viongozi watakaohudhuria mkutano huo utakaoanza Septemba 23, kuleta mipango ya vitendo badala ya hotuba tu.

afpe, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi