1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres azitaka Israel, Hamas kusitisha mapigano

7 Mei 2024

Umoja wa Mataifa umeziomba Israel na Hamas kutopoteza fursa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, wakati Israel ikitwaa kile inachosema ni "udhibiti wa kiuendeshaji" wa mji wa kusini mwa Gaza, Rafah.

Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezitolea wito Israel na Hamas kutoacha fursa ya sasa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.Picha: ZUMA Wire/IMAGO

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York siku ya Jumanne (Mei 7), Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, aliita siku hiyo kuwa siku ya wasiwasi mkubwa, akimaanisha hatua iliyochukuliwa na Israel kutuma vifaru vyake kwenye mji wa Rafah unaowahifadhi mamilioni ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, hata baada ya raia kushinda usiku kucha wakishangiria tamko la kundi la Hamas la kukubali pendekezo la kusitisha mapigano.

"Leo nimetuma ombi la dhati kwa serikali ya Israel na kwa uongozi wa Hamas ili wende mbele zaidi kuyatia uhai makubaliano haya ambayo kwa kweli ni muhimu sana. Hii ni fursa ambayo haiwezi kupotezwa. Na uvamizi wa ardhini dhidi ya Rafah utakuwa jambo lisilovumilika kwani madhara yake yatakuwa makubwa sana kwa raia na kwa sababu ya athari yake ya kuliingiza eneo zima la Mashariki ya Kati kwenye hatari." Alisema.

Soma zaidi: Raia wengi wa Gaza wanakimbilia eneo la mpakani na Misri wakihofia mapigano kati ya Israel na Hamas

Guterres alionya kuwa endapo Israel ingeliendelea na mpango wake wa kuivamia Rafah ingelikuwa imetenda kosa la kimkakati, janga la kisiasa, na italeta jinamizi la kibinaadamu. 

Mmoja wa Wapalestina walioondoka mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah baada ya kuamriwa kufanya hivyo na Israel siku ya Jumatatu (Mei 6, 2024).Picha: AFP via Getty Images

"Kufungwa kwa vivuuko vya mipaka ya Rafah na Karem Shalom kunaathiri huduma za kibinaadamu ambazo tangu hapo ni za kiwango cha chini", alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akitowa wito wa kufunguliwa tena mara moja kwa vivuuko hivyo.

Msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa Huduma za Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), Jens Laerke, aliewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba walikuwa wamezuiwa na mamlaka za Israel kuvuuka mpaka wa Rafah, wakiambiwa kusingekuwa na upitishaji wa watu, bidhaa wala vifaa vyovyote kwa sasa.

Misri yasema wajumbe wa majadiliano wamewasili Kairo

Kwa upande mwengine, Misri ilisema wajumbe wa Marekani, Qatar na Hamas walikuwa tayari wamewasili mjini Kairo kwa ajili ya kuendeleza majadiliano ya kupata mkataba wa kusitisha mapigano. Hayo ni kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al-Qahera, ambacho kina mafungamano na serikali ya Misri.

Barani Ulaya, mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu walikamatwa na polisi katika mataifa mbalimbali baada ya kuanzisha kambi za kupinga mauaji ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, wakifuata mfano wa wenzao wa Marekani.

Baadhi ya mahema yaliyojengwa na wanafuzi wa Chuo Kikuu Huru cha mjini Berlin, Ujerumani kupinga mauaji yanayoendelea Ukanda wa Gaza.Picha: Cuneyt Karadag/Anadolu/picture alliance

Soma zaidi: Israel yathibitisha mateka walioachiliwa na Hamas

Kwenye mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, polisi iliwatawanya na kuwakamata wanafuzi kwenye Chuo Kikuu Huru, baada ya wanafunzi hao kujenga mahema yapatayo 20 kwenye uwanja wa chuo hicho.  

Mapema ya hapo, polisi walivunja maandamano kama hayo kwenye Chuo Kikuu cha Amsterdam nchini Uholanzi na kuwatia nguvuni wanafunzi 140, kwa mujibu wa msemaji wa polisi ya nchi hiyo, Sara Tillart. 

Maandamano kama hayo yameshuhudiwa kwenye vyuo vikuu  mbalimbali vya Finland, Denmark, Italia, Uhispania, Ufaransa na Uingereza katika siku za hivi karibuni.

Vyanzo: Reuters, AFP, AP