1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Dunia yahitaji mkakati wa ulimwengu kuhusu chanjo

Yusra Buwayhid
18 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekosoa vikali usambazaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 usiozingatia haki na usawa. Amesema mataifa 10 ndiyo yaliyotumia asilimia 75 ya chanjo hadi sasa.

UNTV Videostill | Konferenz: UN Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: UNTV/AP/picture alliance

Guterres ameyasema hayo jana katika mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ameutaka ulimwengu kuchukua hatua za kuhakikisha kila mtu katika kila taifa ulimwenguni kote anapatiwa chanjo haraka iwezekanavyo. 

Ameongeza kwamba kuna mataifa 130 ambayo hadi hivi sasa hamna hata mtu mmoja aliyepewa chanjo ya kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo unaotokana na virusi vya corona. Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza lazima hali hiyo ibadilike haraka iwezekanavyo.

Chanjo inaleta matumaini 

"Utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unatupa matumaini makubwa. Lakini katika wakati huu mgumu kuzingatia usawa katika kutoa chanjo hiyo ndiyo jambo muhimu zaidi ulimwenguni kote. Lazima tuhakikishe kila mtu, kila mahali, anachanjwa haraka iwezekanavyo," amesema Guterres.

Guterres ametoa wito wa kuundwa mpango wa haraka wa kutoa chanjo ulimwenguni kote utakawakutanisha wale walio na nguvu ikiwa ni pamoja na; wanasayansi, watengenezaji wa chanjo na wale ambao wanaweza kufadhili mpango huo, ili kuhakikisha kila mwanadamu ana haki sawa ya kupata chanjo.

Moja ya chanjo ya virusi vya coronaPicha: Md Rafayat Haque Khan/Zuma/picture alliance

Aidha, Guterres amelitaka kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani G20 kuanzisha kikosi maalumu cha dharura ambacho kitasimamia usambazaji wa chanjo hiyo pamoja na ufadhili wake. Amesema kikosi kazi hicho kinapaswa kuwa na uwezo wa kuzihamasisha kampuni zinazotengeneza madawa pamoja na wadau wengine kwenywe sekta hiyo.

Uhamasishaji wa kukusanya fedha

Guterres amesema mkutano wa kesho Ijumaa wa kundi la mataifa saba makuu yaliyostawi kiuchumi ambayo ni; Marekani, Ujerumani, Japan, Uingereza, Ufaransa, Canada na Italia, unaweza kuanza kuhamasisha ukusanyaji wa fedha zitakazohitajika kutekeleza mpango huo utakaounufaisha ulimwengu mzima.

Mawaziri 13 walihutubia jana katika mkutano huo wa baraza la usalama ulioandaliwa na Uingereza kwa lengo la kutafuta njia za kuboresha utoaji wa chanjo ya COVID-19, ikiwa ni pamoja na kwenye maeneo yenye mizozo.

Soma zaidi: Mataifa maskini kuanza kupelekewa chanjo ya COVID-19

Watu wapatao milioni 109 wameambukizwa virusi vya corona na wengine milioni 2.4 wamefariki dunia kutokana na maambukizi hayo. Huku kasi ya kutengeneza chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 ikiwa inazorota, mataifa mengi hasa yaliyo maskini yanalalamika kuwa yamesahauliwa na kuwekwa nyuma kwenye suala la chanjo. Lakini hata mataifa tajiri nayo pia yanalalamika juu ya kasi ndogo ya makampuni ya madawa ya kuzalisha chanjo hiyo.

(AFP, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW