1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Guterres: Haki za binaadamu zinadhoofishwa na vita

27 Februari 2023

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa linajizatiti kuimarisha mchakato wa kufuatilia madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Urusi nchini Ukraine katika kikao kinachokutanisha mataifa 47 wanachama.

Schweiz, Genf | António Guterres im UN-Menschenrechtsrat
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Mkuu wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa amelaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, wakati akifungua kikao cha baraza hilo ambacho miongoni mwa masuala mengine, wajumbe wake wanataka kuimarisha mchakato wa kufuatilia madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Urusi nchini Ukraine, huku China ikitilia mkazo kutafutwa suluhu ya mzozo huo kwa njia ya mazungumzo. 

Katika moja ya hotuba zake mbele ya mataifa wanachama 47, Volker Turk, kamishna mkuu wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa hakusita kulaani vikali uvamizi huo wa Urusi nchini Ukraine na kuonya kwamba hata zile hatua zilizopigwa katika masuala ya haki za binaadamu sasa zinarudishwa nyuma, akiuangazia hasa uvamizi wa Urusi na kuufananisha na ukandamizaji.

Si yeye tu aliyelaani ukiukaji wa haki za binaadamu, bali hata katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonia Guterres alisema kwenye hotuba nyingine kwamba vita vimechochea ukiukwaji mkubwa wa haki.

"Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umechochea ukiukwaji wa haki za binadamu tulizonazo hii leo. Umechochea vifo vingi, uharibifu na ukosefu wa makazi. Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu imerekodi visa vingi vya ukiukwaji kama unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanaume, wanawake na wasichana kwenye maeneo ya migogoro, pamoja na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu, watu kulazimishwa kupotea na raia kuwekwa kizuizini kiholela.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ameyataka mataifa kuwa wavumilivu wakati wakiendelea kuchukua hatua dhidi ya Urusi Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesisitizia umuhimu wa Baraza hilo akiangazia visa vya ukiukwaji vinavyodaiwa kufanywa na Urusi, Iran, Afghanistan na mataifa mengine. Aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin kabla ya kuondoka kwenda kuhudhuria kikao hicho huko Geneva kuwa ingawa wengi wanahisi utekelezwaji wa hatua za baraza hilo unakwenda taratibu, lakini kila azimio, kila tume ya uchunguzi inayoundwa na kila mjumbe maalumu anayeteuliwa ni sawa na tofali linalounda ukuta thabiti zaidi unaotenganisha ukweli na uongo.  

China yasisitiza suluhu ya amani.

Tukisalia kwenye masuala yahusuyo Ukraine, China imesisitiza kwa mara nyingine hii leo kwamba ingependelea suluhisho la amani na mazungumzo kuelekea mzozo kati ya Urusi na Ukraine licha ya Onyo la Marekani kwamba Beijing huenda ikawa inaangazia kuisaidia kijeshi, mshirika wake Urusi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amesema wamekuwa wakifanya mawasiliano na pande zote juu ya mzozo huo ikiwa ni pamoja na Kyiv na kusisitiza kwamba msimamo wake uko wazi.

Huko Moscow, msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema mchana wa leo kwamba mkakati wa China unatakiwa kuchambuliwa kwa kina na maslahi ya pande zote kuzingatiwa, ingawa hadi sasa Moscow haijaona dalili yoyote inayoashiria uwezekano wa suluhu kwa njia ya amani.

Na huko New Delhi taarifa zinasema mawaziri wa mambo ya nje kutoka kutoka mataifa yaliyondelea na yanayoinukia kiuchumi ulimwenguni wiki hii watakusanyika mjini humo, katika mkutano utakaogubikwa na kiwingu cha mzozo wa Urusi na Ukraine pamoja na wasiwasi unaoletwa na mvutano kati ya China na Marekani. Mkutano huo wa G20 unaofanyika Machi Mosi na mbili, utawakutanisha ana kwa ana mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, Sergei Lavrov wa Urusi na James Clevery wa Uingereza na waziri wa mambo ya nje wa China, Qin Gang. 

Julai mwaka jana, waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov alisusia mkutano kama huo uliofanyika Bali baada ya mataifa ya magharibi kulaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Soma Zaidi: Maoni: Uvamizi wa Urusi Ukraine unamhusu kila raia wa Ulaya