Guterres: Iokoweni dunia ama tutaangamia sote
1 Novemba 2021Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amewaambia viongozi wa dunia kwamba kushikwa kwenye kongamano la kimataifa juu ya kupanda kwa joto ulimwenguni kutamaanisha kwamba kila mwaka watapaswa kuja na ahadi mpya badala ya kuzingatia ratiba ya sasa ya kila baada ya miaka mitano.
Akizungumza kwenye kongamano hilo lililofunguliwa leo (Novemba 1), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema endapo ahadi za mataifa makubwa kwenye mkutano huo hazitakidhi mahitaji yaliyopo, dunia haitakuwa na muda mrefu wa kuishi.
"Tunakabiliwa na uchaguzi mgumu: Ama tuyasimamishe mabadiliko ya tabianchi, ama yatusimamishe sisi. Umewadia wakati wa kusema imetosha. Imetosha kuungamiza mfumo wa bioanuwai. Imetosha kujiuwa wenyewe kwa hewa ya ukaa. Imetosha kuyafanya mazingira kama ni choo. Imetosha kuchoma na kuchimba na kukokozowa madini chini huko aridhini. Tunachima makaburi yetu wenyewe," alisema katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
"Daima kumekuwa na nakisi kwenye ukweli na hali ya kuaminika na ziada kwenye mkanganyiko malengo ya upunguzwaji wa gesi chafu na kuondoshwa kwake kabisa." Aliongeza.
Mkuu wa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Umoja huo umeandaa kundi la wataalamu kupima na kuchambuwa ahadi za kukomesha kabisa uzalishaji wa gesi chafu kwa makundi yanayohusika na uzalishaji huo na ambayo si serikali.
Matajiri wawasaidie masikini kuachana na CO2
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema kwamba sekta binafsi inahitajika kuzisaidia nchi masikini kuzifanya chumi zao zisitegemee tena uzalishaji wa gesi chafu, akirejelea kauli yake kwamba mkutano huu wa Umoja wa Mataifa mjini Glasgow utafanikiwa.
Johnson aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba dunia ina wajibu wa kupata dola bilioni 100 kwa mwaka, ambazo ziliahidiwa na mataifa yaliyoendelea mwaka 2020, lakini sasa zinategemewa kuwasilishwa mwaka 2023.
"Lakini hatuwezi na hatutafanikiwa hilo kama serikali pekee. Humu kwenye ukumbi tunaweza kutoa mabilioni, hakuna shaka. Lakini makampuni yana matrilioni, na sasa ni jukumu letu kushirikiana kuwasaidia marafiki zetu kuachana na shughuli zinazozalisha hewa chafu," alisema waziri mkuu huyo wa Uingereza.
Johnson alikuwa ameifananisha ya dunia ilivyo na filamu ya James Bond, ambaye alikuwa akiwania kukipata kifaa kinachoweza kuungamiza ulimwengu ili kukinasuwa, akisema ndivyo ilivyo kwa viongozi wa dunia wanaokusanyika sasa mjini Glasgow, wakiwa na ulazima wa kukikanuwa kifaa hicho kabla ya sayari ya dunia kuangamia.
Zaidi ya viongozi 130 wa dunia wanahudhuria kongamano hili litakaloendelea kwa wiki mbili nzima kusaka njia ya kuhakikisha kuwa vipengele muhimu vya makubaliano ya mwaka 2015 yaliyofikiwa Paris, Ufaransa, vinatekelezwa kikamilifu. Miongoni mwa vipengele hivyo ni kuweka ukomo wa kiwango cha joto duniani kufikia nyuzi 1.50 za Celcius na kushusha kiwango cha uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia sifuri hapo mwaka 2050.