1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Guterres: Mashariki ya Kati iko katika ukingo wa vita

15 Aprili 2024

Mashambulizi ya moja kwa moja kutoka Iran dhidi ya Israel yameyaweka mataifa hayo mawili kwenye ukingo wa vita mnamo wakati hofu ya uwezekano wa vita kuenea kote Mashariki ya Kati ikitanda.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: Yuki Iwamura/AP Photo/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kutuliza hali katika Mashariki ya Kati. Mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel yamewachochea viongozi mbalimbali ulimwenguni kote kutoa wito wa pande zote husika kujizuia na kupunguza uhasama, 

Hayo yanajiri baada ya mashambulizi ya moja kwa mojayaliyofanywa na Iran dhidi ya Israel, usiku wa kuamkia Jumapili, kulipiza kisasi kutokana na shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.

Akizungumza kwenye kikao maalum cha Umoja wa Mataifa huko mjini New York, Guterres amesema raia wa Mashariki ya Kati wanakabiliwa na hatari halisi ya mzozo wa kiwango cha juu. Kikao hicho kiliitishwa kufuatia ombi la Israel baada ya mashambulizi ya angani Iran dhidi yake.

"Ni muhimu kuepusha hatua yoyote inayoweza kusababisha makabiliano makubwa ya kijeshi yanayohusisha pande mbalimbali katika Mashariki ya Kati. Tayari raia wanakabiliwa na mzigo mkubwa na wanalipa gharama ya juu zaidi. Tuna jukumu la pamoja kushirikisha pande zote husika ili kuzuia machafuko kuongezeka zaidi," amesema Guterres.

Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wa mataifa saba tajiri zaidi duniani kidemokrasia na kiviwanda maarufu kama G-7, waliishutumu Iran kwa mashambulizi hayo, huku wakielezea uungwaji wao mkono kwa usalama wa Israel.

Kwenye taarifa yao ya pamoja viongozi wa G-7 wamesema, kufuatia hatua yake, Iran imepiga hatua zaidi kuelekea kudhoofisha utulivu wa eneo hilo na hatari ya kuzuka kwa mzozo wa kikanda usioweza kudhibitiwa.

Kulingana na jeshi la Israel, kati ya droni 170 na makombora 30 zilizorushwa na Iran, hakuna hata moja iliyofika Israel, likisema lilifanikiwa kuzuia shambulizi hilo.

Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagari, alielezea kufanikiwa kwa ushirikiano wao na washirika katika kudungua droni za Iran na makombora yake.

"Shambulio la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa lilikabiliwa na ulinzi usio kifani. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa muungano huo kufanya kazi pamoja dhidi ya tishio la Iran na washirika wake katika Mashariki ya Kati," amesema Hagari.

Hagari amesema bado wako ange na wanaendelea kutathmini hali akiongeza kuwa katika saa chache zilizopita wameidhinisha mipango ya operesheni ya mshambulizi na ulinzi.

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

02:41

This browser does not support the video element.

Soma pia: Mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel yalaaniwa kimataifa

Hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliitisha mkutano wa Baraza lake la Mawaziri wa Vita, kuamua kuhusu hatua yoyote ya kuchukua dhidi ya Iran. Hayo ni kulingana na chanzo cha habari katika serikali ya Israel.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameitaka Israel kujizuia baada ya kufanikiwa kuzuia mashambulizi ya Iran.

Naye rais wa Marekani Joe Biden amemtaka Benjamin Netanyahu kutathmini kwa makini hatua yoyote ya Israel ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran, pamoja na athari zitakazojitokeza.

Baraza la Usalama la Iran limeionya Israel dhidi ya hatua yoyote ya kijeshi ya kulipiza kisasi, likisema hatua yoyote ya kijeshi itajibiwa mara kumi zaidi ya mashambulizi yao ya juzi.

Vyanzo: APTN, DPAE, AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW