Guterres: Hali inaendelea kuwa mbaya Ethiopia
18 Oktoba 2022
Tahadhari ya kimataifa imekuwa ikiongezeka kutokana na kushadidi kwa mapigano huko Tigray, ambapo vikosi vya serikali ya Ethiopia na wanajeshi kutoka nchi jirani ya Eritrea wakiongeza mashambulizi karibu na mji wa Shire.
Guterres amewaambia wanahabari katika Umoja wa Mataifa kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya huku ghasia na uharibifu vikifikia viwango vya kutisha. Guterres ameongeza kusema, kuwa uhasama katika eneo la Tigray unapaswa ukomeshwe sasa ikiwa ni pamoja na kuondolewa mara moja na kutengwa kwa vikosi vya Eritrea.
Umoja wa Ulaya na Marekani zatoa wito wa kusitisha mapigano
Umoja wa Ulaya na Marekani pia zimetoa wito wa dharura wa kusitisha mapigano, kufuatia wito wa Umoja wa Afrika wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo na bila masharti.
Mnamo siku ya Jumapili, mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alizihimiza pande zinazohasimiana kujitolea tena katika mazungumzo baada ya kukubali mwaliko wa mazungumzo ya amani nchini Afrika Kusini ambayo yalikosa kufanyika .
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia imeihimiza Ethiopia na Eritrea kusitisha mara moja mashambulizi yao na kutoa wito kwa Etitrea kujiondoa na kwa wapiganaji wa Tigray kukomesha uchochezi wowote zaidi.
Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ametoa ombi sawa na hilo, na katika taarifa yake, amesema anasikitishwa na ongezeko kubwa la ghasia na gharama kubwa kwa maisha ya binadamu isiyoweza kurekebishika.
Serikali ya Ethiopia yaahidi kuchunguza matukio
Serikali ya Ethiopia imesema kuwa inasikitishwa sana na madhara yoyote ambayo huenda yamewakumba raia ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa misaada na kuongeza kuwa itachunguza matukio hayo.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameshutumu pande zote katika mzozo huo kwa ukatili ambao unaweza kuwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Katika taarifa hapo jana, serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ilisema kuwa imejitolea kusuluhisha mzozo huo kwa amani kupitia mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Umoja wa Afrika bila ya kuzungumzia wito wa kusitisha mapigano.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa pia itafuatilia hatua za kinga kulinda uhuru na uadilifu wa Ethiopia dhidi ya vitisho vya ndani na nje na kulishtumu kundi la wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF kwa kushirikiana na mataifa ya nje yenye uadui ambayo hayakutajwa.
TPLF yajibu taarifa ya Abiy Ahmed
Waziri huyo mkuu amesema kutokana na hilo, ni muhimu kwa serikali ya Ethiopia kuchukuwa mara moja udhibiti wa viwanja vyote vya ndege na taasisi nyingine za serikali.
Akijibu taarifa hiyo, msemaji wa kundi la TPLF Getachew Reda, ameliambia shirika la habari la AFP kupitia ujumbe kwamba hii ni ishara wazi kwamba serikali hiyo na washirika wake itafanya kila iwezalo kutekeleza nia yao ya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Tigray.