"Habari za uongo", kitisho cha uhuru wa vyombo vya habari
3 Mei 2019Ongezeko kubwa la taarifa za uongo na za kupotosha ni mada zinazojadiliwa sana katika siku hii ya vyombo vya habari. Hata hivyo wachunguzi wanasema hakuna bara ambalo limesalimika katika suala hili.
Ongezeko la wimbi la taarifa za uongo na taarifa ambazo sio sahihi ni mada zinazojadiliwa katika wiki ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo inaadhimishwa kwa ngazi ya dunia nchini Ethiopia, nchi ambayo ni mwenyeji wa tukio hilo baada ya kuwaacha huru waandishi habari waliofungwa gerezani kama sehemu ya mageuzi yanayoendelea nchini humo. Wakati dunia inafanya maadhimisho ya uhuru wa habari, wafanyakazi wa vyombo vya habari na wataalamu wameonesha wasiwasi wao na kujadili njia za kupambana na taarifa za uongo ambazo wanasema zimekuwa "tishio dhidi ya demokrasia."
Uhusiano kati ya vyombo vya habari na demokrasia ndio kauli mbiu kuu mwaka huu, ambapo zaidi ya matukio 100 yatafanyika duniani kote. Siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu inafanyika kwa mara ya kwanza nchini Ethiopia , nchi ambayo imekuwa ikishutumiwa kwa muda mrefu kwa kuwafunga waandishi habari hadi pale waziri mkuu Abiy Ahmed alipoingia madarakani Aprili , 2018. Serikali yake imewaacha huru waandishi kadhaa waliokuwa kifungoni.
Kielelezo cha uhuru wa habari
Katika taarifa yake kuhusu kielelezo cha Uhuru wa habari duniani shirika la waandishi wasio na mipaka RSF, limesema bara la Ulaya kwa kiasi kikubwa ni sehemu ambayo uhuru wa vyombo vya habari unatekelezwa kwa kiasi kikubwa. Lakini pia ripoti hiyo imesema baadhi ya waandishi isiwafanya wafumbie macho ukweli kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, bwawa limevunjika na nguzo hii ya demokrasia imeathirika pakubwa.
Jamal Khashoggi, Daphne Caruana Galizia, Jan Kuciak, mauaji dhidi yao ni miongoni mwa mashambulio makubwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na ishara ya matatizo makubwa, anasema hivyo Christophe Deloire wa kundi la waandishi wasio na mipaka.
Karibu mtu mmoja kati ya wawili duniani hawapati taarifa huru zinazoripotiwa. Mauaji ya Khashoggi mjini Istanbul yameonesha kuhusu matumizi makubwa ya nguvu yanayotumiwa na baadhi ya nchi dhidi ya waandishi habari.
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban anatumia mbinu za kutokuwa na uaminifu kwa faida zake na kuelezea madai ya 'taarifa za uongo' kuhalalisha kukataa kwake kuzungumza na vyombo vya habari ambavyo haviungi mkono chama chake.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Jeremy Hunt amewaambia waandishi habari mjini Addis Ababa kuwa uhuru wa vyombo vya habari sio maadili ya mataifa ya magharibi ama kitu cha anasa kwa mataifa yanayoendelea.