Hadithi: Urithi unaotoweka mbele ya macho yetu
17 Agosti 2026
Hadithi za wanyama, mashujaa, bahari na viumbe wa ajabu hazikuwa burudani pekee; zilikuwa darasa la maadili, historia na lugha. Lakini leo, mwanga wa simu na televisheni umechukua nafasi ya moto wa jiko na vikao vya hadithi. Je, teknolojia imeufifisha utamaduni huu wa asili, au imeupa sura mpya?
Katika jamii nyingi za Zanzibar, kusimulia hadithi kulikuwa sehemu ya malezi. Watoto walifundishwa kuwaheshimu wakubwa, kuwa waaminifu, kufanya kazi kwa bidii na kuepuka tabia zisizokubalika. Kupitia simulizi, kizazi kimoja kilikabidhi kingine kumbukumbu za ukoo, mila na maisha ya visiwani.
Watoto waliwekwa pamoja nyakati za usiku
Lakini kasi ya maisha ya sasa imebadilisha mpangilio huo. Wazazi wengi wanarejea nyumbani wakiwa wamechoka, huku watoto wakitumia muda mwingi kwenye simu, mitandao ya kijamii na vipindi vya televisheni. Nafasi ya kukaa pamoja na kusikilizana imekuwa ndogo.
Dokta Zainab Ali Iddi, mtaalamu wa lugha ya Kiswahili anasema wazee walitumia nyakati za usiku kuwaweka pamoja watoto na kuwasimulia hadithi kama sehemu ya utamaduni na mafunzo pia.
Kulingana na Dokta Zainab, zamani wakati babu, bibi au shangazi anaanza kusimulia hadithi alikuwa anasema 'Paukwa' na kisha watoto wanaitikia kwa kusema 'Pakawa'. Na wazee wangine walianza kwa kusema 'Hadithi Hadithi, Hadithi Njoo, Uongo njoo, Utamu Kolea'!
''Leo tuzungumzie hadithi zilikuwa zikitambwa hapo zamani walianza pia kwa kusema hapo zamani za kale aliondokea, japokuwa kuna namna nyingine ya kuanza kusimulia hadithi. Mara nyingi wazee wetu walikuwa wakitamba hadithi wakati wa usiku, kwa sababu ni muda wa mapumziko, familia zikikusanyika pamoja na ndiyo watoto wakishirikiana na kukaa pamoja na wakati wanasubiri chakula ndio zikitambwa hadithi,'' alifafanua Dokta Zainab.
Hadithi nyingi hivi sasa zinapatikana kwenye mitandao ya kijamii kama vile TikTok au YouTube. Lakini zile za babu na bibi ambazo zilizokuwa zikitolewa kwa hisia, hazishuhudiwi tena katika nyumba nyingi kwa kuwa sasa kila mtu ana simu yake ya mkononi.
Teknolojia yachangia kufifisha utamaduni huu
Khamis Ali, mkaazi wa Bububu, anasema mabadiliko ya kiulimwengu na kiteknolojia yamesababisha utamaduni wa wazee kuwasimulia watoto hadithi kufifia. Akizungumza na DW, Ali anasema huko ni kupoteza utamaduni wao na asili ya wazazi wao kuwasimulia hadithi za paukwa pakawa.
Katika baadhi ya shule na vikundi vya sanaa Zanzibar, juhudi za kuhuisha utamaduni huu tayari zinaendelea. Vijana wanahimizwa kuandika hadithi za wazee wao, kuziigiza jukwaani na kuzitengeneza kwa mfumo wa sauti au video. Hii inaonyesha kuwa simulizi zinaweza kubadilika bila kupoteza ujumbe wake.
Kwa baadhi ya wazee, kinachopotea si hadithi pekee, bali ni lugha na ukaribu wa kifamilia. Hadithi za jadi hutumia misemo, mafumbo na maneno ya Kiswahili cha kale ambayo hayapatikani kwa urahisi katika mawasiliano ya kila siku. Aziza Khamis na Fatma Ali wakaazi wa visiwani Zanzibar, wanasema wahajawahi kuketi na bibi, lakini wamezisikia kwa walimu wao.
Kwa mujibu wa Aziza, hadithi za paukwa pakawa amezisikia alipokuwa anasoma shule ya msingi, lakini nyumbani hajawahi kuzisikia zikihadithiwa. Kwa upande wake, Fatma anasema hadithi za paukwa pakawa amezisikia tangu alipokuwa shule ya vidudu, lakini baada ya hapo hakuwa wakiwekwa na wazazi na kuzisikia. Lakini kwa sasa anazinasikia hadithi hizo kupitia mitandao ya kijamii kama vile YouTube, Facebook na TikTok.
Wataalamu wa utamaduni wanaona teknolojia si lazima iwe adui wa simulizi za jadi. Simu zinaweza kurekodi sauti za wazee, kuhifadhi hadithi na kuzifikisha kwa vijana walioko mbali. Mitandao ya kijamii, podikasti na video fupi vinaweza kuwa majukwaa mapya ya kusimulia hadithi ikiwa maudhui yake yataandaliwa kwa lugha inayowavutia vijana.
Ili hadithi zidumu zinahitaji kusimuliwa zaidi
Changamoto kubwa ni kuhakikisha hadithi hazigeuki kuwa bidhaa ya burudani isiyo na mizizi. Kamishna wa Utamaduni Zanzibar, Omar Salum, anasema ili hadithi zidumu, zinahitaji kusimuliwa katika familia, kufundishwa shuleni na kupewa nafasi katika matamasha ya sanaa na vyombo vya habari.
''Wazazi, walezi na wazee walizitumia sana hadithi simulizi, yaani hadithi za paukwa pakawa katika kuwafunza watoto wao. Ziliwajenga watoto katika malezi kama vile kuwa wapole, wakarimu, busara na kuwa na utu. Tofauti sana na siku hizi wazee wanawaachia simu watoto ambapo huzitumia kujifunza mengi ya jamii nyengine ambayo yapo kinyume kabisa na maadili yetu na hivyo huchangia kuporomosha maadili yetu kwa ujumla,'' alisisitiza Dokta Omar.
Utamaduni wa kusimulia hadithi haujapotea kabisa; unaonekana kupungua na kubadilisha makazi. Kutoka kibarazani hadi kwenye skrini. Swali si kama teknolojia itachukua nafasi ya hadithi za jadi bali ni kama jamii itaamua kuitumia teknolojia kuziokoa. Kwa sababu hadithi inaponyamazishwa, si sauti ya babu au bibi pekee inayopotea; ni sehemu ya utambulisho wa jamii nzima.