1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadja Lahbib yuko Goma kutathimini hali ya kibinaadamu

20 Februari 2026

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na misaada ya kibinadamu na usimamizi wa migogoro, Hadja Lahbib, yuko ziarani mjini Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akitokea Kinshasa, Bujumbura na Kigali.

Frankreich Straßburg 2026 | Pressekonferenz mit Hadja Lahbib im Europäischen Parlament
Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na misaada ya kibinadamu na usimamizi wa migogoro, Hadja LahbibPicha: Valentine Zeler/European Union

Mashariki mwa DRC, mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya. Majeruhi wa vita, wakimbizi wa ndani, na upatikanaji mdogo wa huduma huku wahudumu wa misaada wakifanya kazi katika mazingira yanayozidi kuwa magumu. Katika ziara yake rasmi, Kamishna wa Umoja wa Ulaya Hadja Lahbib amekuja kujionea hali halisi ilivyo.

Baada ya mikutano ya kikanda, ameongeza mazungumzo na wadau wa ndani, yakiwemo mashirika ya kimataifa ya MSF, INSO na mashirika kadhaa ya ndani ya Kongo. Kwa ujumla, mazungumzo hayo yamebainisha kuwa hali ni ya kutia wasiwasi, kwani kurejea kwa mzozo wa usalama, upatikanaji wa misaada ya kibinadamu umepungua.

Kwa mujibu wa wahudumu wa misaada, baadhi ya maeneo bado hayafikiki. Elisabeth Musafiri, mtetezi wa haki za wanawake, anasema hali ni mbaya kwa wahudumu wa misaada, lakini bado ana matumaini kuwa ziara hii italeta matokeo mazuri:

"Kama watetezi wa haki za binadamu, ninaamini ziara ya Kamishna wa Umoja wa Ulaya inatupa tena matumaini. Kwa wahudumu wa misaada, imekuwa ngumu sana. Hali ni mbaya sana. Lakini bado tunatumaini atafanya utetezi na kwamba mwisho wa mgogoro huu, walengwa wa misaada watapata tena matumaini. Usalama upo, lakini bado kuna vikwazo vingi kutoka kwa wale wanaoongoza sasa mji wa Goma.”

Waasi wa M23 wakiwa mjini Goma Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Katika ziara yake, Kamishna wa Umoja wa Ulaya alitembelea hospitali ya CBCA Ndosho inayoungwa mkono na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.  Mwisho wa ziara yake, alizungumzia ahadi alizopata kutoka pande mbalimbali, na katika ngazi ya juu zaidi alikutana na viongozi wakuu wa harakati ya kisiasa na kijeshi wa AFC/M23, inayodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa:

"Hali ni mbaya sana. Tunatoa msaada mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani katika ukanda wa Maziwa Makuu. Lakini tunahitaji kusaidiwa ili tufanye kazi yetu. Kuna ongezeko la ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu, wafanyakazi wetu wanahatarisha maisha yao ili kuokoa ya wengine, mashirika ya kimataifa na yale ya Umoja wa Mataifa yanafanya kazi katika mazingira magumu.

Hapa nimepata ahadi za vitendo kutoka kwa pande zote nilizokutana nazo, na ninatumaini ahadi hizo zitatekelezwa na kwamba ujumbe huu utazaa matunda.”

Sasa inabaki kuonekana kama ahadi hizo zitageuzwa kuwa vitendo, lakini kwa wananchi walioathirika mjini Goma na kote mashariki mwa DRC, dharura ya kibinadamu haiwezi kusubiri.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW