1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Haiti hatimaye yaunda rasmi Baraza tawala la mpito

Sylvia Mwehozi
13 Aprili 2024

Haiti hatimaye imeunda rasmi Baraza tawala la mpito lililopewa jukumu la kujaza pengo la uongozi nchini humo na kurejesha hali ya utulivu kufuatia ghasia zilizozuka za magenge ya kihalifu.

Haiti | Port-au-Prince
Maafisa wa polisi wakilinda doria mji mkuu wa Port-au-PrincePicha: Clarens Siffroy/AFP

Amri ya kuundwa kwa baraza hilo imetangazwa siku ya Ijumaa kupitia gazeti rasmi la "Le Moniteur", mwezi mmoja baada ya Waziri Mkuu Ariel Henry kusema kuwa atajiuzulu kutokana na wimbi la mashambulizi ya magenge yenye silaha katika mji mkuu wa Port-au-Prince.

Tangazo hilo, ambalo lilikuwa limecheleweshwa kwa wiki kadhaa na mizozo ya kisiasa, ni hatua ya matumaini katika juhudi za kupelekwa kikosi cha polisi wa kimataifa kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa, kikiongozwa na Kenya.

Amri hiyo inalipa baraza hilo jukumu la "haraka" kuteua waziri mkuu mpya na serikali "ikijumuisha" mirengo mbalimbali ya kisiasa ya Haiti. Kuundwa kwa baraza hilo linaloungwa mkono na Marekani pia ni hatua ya kwanza kuelekea kufanyika uchaguzi wa rais ifikapo mwaka 2026.

Raia wa Haiti wakisubiri kuvuka mpaka ili kununua bidhaa Jamhuri ya DominicanPicha: Orlando Barria/EPA

Hata hivyo, maswali bado yamesalia ikiwa serikali ya mpito, iliyopewa jina la Baraza la Mpito la Rais, itaweza kuwa na nguvu dhidi ya magenge ya kihalifu yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu Port-au-Prince.

Sehemu ya amri hiyo ilieleza kwamba "Baraza la Mpito la Raislitatumia mamlaka mahususi ya urais wakati wa kipindi chote cha mpito hadi uchaguzi wa rais, ambao lazima ufanyike kabla ya Februari 7, 2026."

Nchi hiyo haijafanya uchaguzi tangu 2016 na imekuwa bila rais tangu Jovenel Moise alipouawa mwaka 2021. Waziri Mkuu Henry alikuwa nchini Kenya mwezi Februari, akijaribu kuandaa kikosi cha polisi cha kimataifa, wakati magenge yalipoanzisha mashambulizi yaliyoratibiwa na kumtaka ajiuzulu.

Baada ya shinikizo kubwa la Marekani na nchi za kikanda, Henry alikubali kujiuzulu na kuwezesha kuundwa kwa baraza la mpito. Chini ya amri hiyo, Henry sasa atajiuzulu rasmi baada ya baraza hilo kumteua waziri mkuu mpya.

Wafungwa wapatao 4,000 waliachiliwa baada ya magenge kuvamia na kushambulia magereza makubwa mawili ya Haiti. Magenge hayo pia yalishambulia vituo vya polisi na uwanja wa ndege. Nchi kadhaa ikiwemo Marekani na zile za Umoja wa Ulaya ziliwahamisha wanadiplomasia na raia wao huku hali ya usalama ikizidi kuzorota.

Polisi wanapiga doriaPicha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, lilionya kuwa njaa na utapiamlo vinaendelea kushuhudiwa nchini Haiti, ambayo imekuwa ikikabiliwa na athari za tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2010 lililosababisha vifo vya maelfu.

Jumuiya ya kikanda ya nchi za Karibia CARICOM, ambayo imekuwa na jukumu kubwa katika juhudi za kuundwa Baraza la mpito, ilisema kuwa hatua hiyo "inaashiria uwezekano wa mwanzo mpya kwa Haiti."

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haiti imesema "itaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato wa kisiasa wa Haiti," na kuongeza kuwa "uungwaji mkono wa kimataifa kwa polisi wa kitaifa wa Haiti bado ni muhimu katika kurejesha usalama na utawala wa sheria."

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW