1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Huduma na vifaa vya matibabu mashakani Haiti

11 Aprili 2024

Wiki kadhaa za ghasia za magenge ya uhalifu nchini Haiti, zimelazimisha karibu hospitali 18 kuacha kufanya kazi na hivyo kusababisha uhaba wa vifaa na huduma mbaya ya matibabu.

Haiti | Port-au-Prince
Wanajeshi wakionekana kupiga doria katika mji Mkuu wa Haiti Port-au-Prince Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Shirika la misaada ya kibinadamu la The Alliance for International Medical Action lenye makao yake nchini Senegal limeonya kwamba uhaba wa vifaa vya matibabu unatokana na kuendelea kufungwa kwa bandari kuu ya Haiti pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa.

Antoine Maillard, daktari na mratibu wa shirika hilo aliyeko katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince anasema hali ni ngumu mno na inaathiri harakati zao za kila siku. Vurugu za magenge hayo zimesababisha takriban watu 17,000 katika mji mkuu kulazimika kuyahama makazi yao. Wengi wao wamesongamana katika shule na majengo yaliyotelekezwa ambako wanaishi katika mazingira duni na mara nyingi hutumia choo kimoja.

Zaidi ya watu 50,000 wakimbia mji mkuu wa Haiti

Maillard amesema wafanyakazi wa misaada walifanikiwa kufika kwenye kambi moja ya watu waliokimbia makazi yao, lakini walishindwa kutoa msaada kwa watu hao kutokana na milio mingi ya risasi. Wakaazi wa Port-au Prince wanasema hali ni ya kutisha huku wakiitupia lawama serikali.

Ghasia zilimlazimu Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry kutangaza mwezi uliopita kwamba atajiuzulu mara tu baraza la mpito litakapoundwa.

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada huko Haiti wanasema mzozo wa kiafya unazidi kuwa mbaya na imekuwa vigumu kupata dawa za msingi ikiwa ni pamoja na antibiotics na dawa za kuzuia magonja ya kuhara tangu pale magenge ya uhalifu kuwalazimu wauzaji wa dawa hizo kufunga maduka yao. Hata kiwango kidogo cha dawa kinachopatikana basi huwa kwa bei ya juu.

Mexico yawahamisha raia wake 34 kutoka Haiti

Athari za ukosefu wa madawa zaanza kuonekana

Uhaba wa vifaa vya matibabu unatokana na kuendelea kufungwa kwa bandari kuu ya Haiti pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa.Picha: RICARDO ARDUENGO/AFP/Getty Images

Hali hiyo inapelekea Wahaiti wengi kama Denise Duval mwenye umri wa miaka 65 kushindwa kununua dawa zinazohitajika au hata kuonana na daktari. Bi Duval anasema afya yake hivi sasa sio nzuri kwa kuwa anasumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu na mara nyingi huhisi kizunguzungu huku mapigo yake ya moyo yakienda mbio kutokana na kusikia kila mara milio ya risasi. Hata hivyo bibi huyo ana matumaini kuwa hali ya kiusalama itaboreka na kurejea katika hali ya kawaida.

Barabara kuu za Haiti hazipitiki, na Wahaiti wengi kama Nadine Prosper mwenye umri wa miaka 52 wanashindwa kuzifikia hospitali chache zinazofanya kazi. Bi Prosper alipoteza mguu wake wa kushoto wakati wa tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Haiti mnamo mwaka 2010 wa Haiti tetemeko la ardhi, na kwa sasa hawezi kupata dawa anazozihitaji.

Mtaalam wa UN: Haiti inahitaji walinda amani 5,000 kukabiliana na magenge ya wahalifu

Hospitali kubwa na maduka ya dawa yamefungwa kutokana na kuendelea kwa vurugu hizo ambazo maafisa wa afya wanasema ni sawa na vita. Licha ya baadhi ya zahanati na hospitali za kibinafsi kuendelea kufanya kazi, watu wengi katika nchi hiyo ambayo asilimia 60 ya idadi ya watu wana kipato cha chini ya dola 2 kwa siku, hawawezi kumudu gharama za hospitali hizo.

afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW