Viongozi wa Haiti washindwa kuunda serikali ya mpito
26 Machi 2024Hali ya vuta nikuvute ndio imeendelea kushuhudiwa siku ya Jumatatu wakati wa msururu wa mikutano ya Baraza la mpito ambalo litakuwa na jukumu la kumchagua kiongozi mpya wa Haiti. Wanachama wa baraza hilo walikutana jana kwa mazungumzo na viongozi wa jumuiya ya kikanda Caricom, maafisa kutoka Marekani, Canada na Ufaransa.
Pamoja na mambo mengine, baraza hilo bado halijaapishwa kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa wanachama wake.
Soma pia: UN: Raia 33,000 wa Haiti wanakimbia machafuko katika mji mkuu
Mwishoni mwa jumaa, mwanachama mmoja wa Baraza hilo la mpito alijiuzulu baada ya kupokea vitisho vya kuuawa. Balozi wa Haiti katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO Dominique Dupuy, na ambaye alichaguliwa na muungano mmoja wa kisiasa, alitangaza kujiondoa, akitaja vitisho dhidi yake na familia yake pamoja na kauli za dhihaka dhidi ya wanawake.
Baraza la mpito linatakiwa kuundwa na wajumbe saba wenye uwezo wa kupiga kura na wajumbe wawili wasiopewa jukumu hilo na litawajumuisha watu kutoka katika vyama vya siasa vya Haiti, sekta ya kibinafsi na wengineo, na litakuwa na jukumu ya kuchagua waziri mkuu wa muda pamoja na serikali ya mpito ili kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi.
Soma pia: Vitisho vya kuuwawa chanzo cha kutoanzishwa baraza la kumchagua rais Haiti
Mgogoro wa kiusalama nchini Haiti umechochewa pia na hali ya kisiasa. Uchaguzi haujafanyika tangu mwaka 2016, huku Waziri Mkuu Ariel Henry akiliongoza taifa hilo tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mnamo mwaka 2021.
Kufuatia shinikizo la magenge ya uhalifu ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu Port-au- Prince, Waziri Henry alitangaza mnamo Machi 11 mwaka huu kuwa atajiuzulu mara baada ya kuapishwa Baraza la mpito.
Hali mbaya ya kibinaadamu
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba huduma za misaada huko Port-au-Prince bado zinatatizwa na ghasia pamoja na ukosefu wa usalama. Farhan Haq, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mgogoro huo umedumaza shughuli na kukwamisha ufikiaji wa vituo vichache vilivyosalia.
Haq ameongeza kuwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani, chini ya nusu ya vituo vya afya katika mji mkuu wa Haiti vinafanya kazi kikamilifu.
Soma pia: Jukumu la kihistoria la Ufaransa katika mzozo wa Haiti
Tangu Februari 29 kulipoibuka vurugu mpya nchini Haiti, makumi ya watu wameuawa huku wengine zaidi ya 33,000 wakilazimika kuuhama mji mkuu Port-au-Prince. Magenge ya wahalifu yamevamia vituo vya polisi, uwanja wa ndege ambao bado umefungwa pamoja na gereza kuu mbili na kuruhusu kuachiliwa kwa watu zaidi ya 4,000. Kutokana na hali hiyo, nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Ufaransa na Canada zimeanza kuwahamisha raia wao.
(AFP,AP)