1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti yaomba wanajeshi wa kigeni kutoka Marekani

Yusra Buwayhid
10 Julai 2021

Baada ya mauaji ya Rais Jovenel Moise, Haiti imeomba wanajeshi wa kigeni kulinda bandari zake, viwanja vya ndege na miundombinu mingine. Marekani na Umoja wa Mataifa bado hazijatangaza kuipatia msaada wa kijeshi.

Haiti - Ermordung des Präsidenten Jovenel Moise
Picha: Estailove St-Val/Reuters

Serikali ya mpito ya Haiti Ijumaa imeiomba Marekani na Umoja wa Mataifa kuisaidia kulinda usalama kwa kutuma wanajeshi nchini humo, kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moise.

"Kwa hakika tunahitaji usaidizi na tumewaomba washirika wetu wa kimataifa kutusaidia. Tunaamini washirika wetu wataweza kulisaidia jeshi la polisi kuituliza hali nchini Haiti," Waziri Mkuu wa Mpito Claude Joseph ameliambia shirika la habari la AP.

Marekani tayari ilikwisha jitolea kuisaidia Haiti kupitia idara yake ya upelelezi ya FBI siku moja baada ya Moise kuuliwa na watu wawili waliokuwa na silaha walioivamia nyumba yake. Hata hivyo, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani amesema hakuna mipango yoyote ya kuipatia Haiti msaada wa kijeshi kwa sasa.

Soma zaidi: Raia wa Marekani na Colombia washukiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti

Aidha Haiti imeomba msaada wa kijeshi kutoka katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Chombo hicho cha kimataifa bado hakikutoa jibu lake. Shirika la habari la AFP limesema duru za kidiplomasia kutoka Umoja wa Mataifa zimesema kwamba kunahitajika kupitishwa azimio la Baraza la Usalama kuweza kuipatia Haiti msaada uliouomba. 

Haiti | Joseph Lambert spika wa bungePicha: Pierre Michel Jean/AFP/Getty Images

Maafisa wa Haiti wanahofia miundombinu kushambuliwa

"Tulifikiria kwamba mamluki wanaweza kuja kuharibu baadhi ya miundominu ya nchi ili kusababisha ghasia. Katika mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa tuliwasilisha ombi letu hilo," amesema waziri anaesimamia uchaguzi Mathias Pierre.

"Tuko katika hali ambayo imetufanya tuamini kwamba miundombinu muhimu ya nchi kama vile bandari, uwanja wa ndege na vyanzo vya nishati vinaweza kulengwa kwa mashambulizi," ameongeza Pierre.

Watu wapatao 28 inadaiwa kuwa wamehusika na mauaji ya Moise, ikiwa ni pamoja na raia wawili wa Marekani, amesema mkuu wa polisi Leon Charles Alhamisi.

Uongozi wa Moise ulizungukwa na utata tangu alipoingia madarakni mnamo mwezi Februari 2017. Kupanda kwa bei ya mafuta, matatizo ya kiuchumi na jinsi serikali ilivyoshughulikia janga la maambukizi ya virusi vya corona vilichangia kuwahamasisha wananchi kumtaka ajiuzulu katika miaka ya hivi karibuni.

Soma zaidi: Mustakabali wa Haiti mashakani baada ya mauaji ya rais

Kikundi cha maseneta wa Haiti kilimtangaza kiongozi wa Seneti Joseph Lambert kama rais wa muda Ijumaa. Hatua hiyo hata hivyo imepuuzwa na Waziri Mkuu wa mpito Claude Joseph. Umoja wa Mataifa unamzingatia Joseph kama kiongozi halali wa Haiti hadi uchaguzi utakapofanyika baadaye mwaka huu.

Bunge la Marekani lasema mahitaji ya Haiti yapewe kipaumbele

Mbunge wa Marekani Andy Levin, ameiambia DW kwamba Haiti imekumbwa na misukosuko kwa miaka mingi,

"Sidhani kama ni sahihi kusema kwamba usalama wa nchi na wa watu wa Haiti upo mikononi mwa udhibiti wa mtu yeyote," amesema Levin.

"Sisemi kwamba napinga kabisa mwanajeshi wa Marekani kutumwa Haiti, lakini lazima tuchukue tahadhari sana na tushirikiane na watu wa Haiti juu ya namna ya kuwatuma wanajeshi hao pamoja na idadi yao. Na lazima tuchukue hatua katika namna ambayo itairidhisha jamii nzima ya watu wa Haiti."

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW