1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti yahitaji msaada wa dola bilioni nne kujijenga upya

31 Machi 2010

Nchi 120 na mashirika ya kimataifa yaahidi kutoa msaada kwa Haiti

Wafadhili wa kimataifa wakiwa katika ufunguzi wa mkutano wa kuisaidia Haiti nchini Marekani.Picha: AP

Haiti hii leo imeomba msaada wa dola bilioni 4 kutoka kwa nchi mbalimbali kote duniani kuisadia kuijengya upya baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mapema mwaka huu lililosababisha vifo vya watu takriban laki tatu.

Wajumbe kutoka nchi 120 pamoja na wa mashirika ya kimataifa na makundi ya  kutoa msaada wanakutana katika afisi kuu za umoja wa mataifa mjini New York nchini Marekani kutoa ahadi za kuisaidia serikali ya Haiti  katika mpango wa ujenzi mpya wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa nafasi za kazi na kuufufua uchumi .

Waziri wa Haiti wa fedha na uchumi Ronald Baudin aliambia shirika la utangazaji la Reuters kwamba Haiti inatarajia kupokea ahadi za msaada wa dola billioni 4 kwa muda wa miaka 3 ambapo wanatarajia dola bilioni 1.3 ziwasilishwe kwa muda wa miezi 18 ya kwanza.

Haiti ilikuwa tayari ni nchi maskini katika kizio cha magharibi ya dunia iliyo na viwango vya juu vya ukosefu wa kazi pamoja na idadi kubwa ya watu wasiojuwa kusoma, kabla ya kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi.

Inakadiriwa kwamba gharama za uharibifu uliotokea kwenye tetemeko hilo kubwa la ardhi ni kati ya dola bilioni 8 hadi 14.

Umoja wa Ulaya pamoja na muungano wa makundi ya misaada ya kibinaadamu nchini Marekani zimeashiiria kwamba huenda zikatoa misaada ya zaidi ya dola bilioni 2.7 huku Rais wa Marekani Barack Obama akiomba bunge lake dola bilioni 2.8 kuisaidia Haiti katika ujenzi huo.

Wakati huo huo afisa mmoja wa juu nchini Marekani  amedokeza kwamba utawala wa Obama kupitia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton utatangaza ahadi ya dola bilioni 1.15 kwa muda wa miaka miwili ijayo.

Umoja wa mataifa unazidi kutoa wito kwa nchi nyingine kusaidia katika kujenga upya serikali ya nchi ya Haiti ambapo kando na wizara moja pekee ofisi za wizara nyingine zote ziliharibika na karibu thuluthi moja ya maafisa wake wa serikali kuuwawa katika tetemeko hilo la ardhi. Mwakilishi mkuu wa Umoja wa mataifa  nchini Haiti Edmont Mulet  alisema, 'Huu ndio wakati wa mabadiliko na kwa jamii ya kimataifa kushirikiana na nchi ya Haiti,na serikali ya Haiti,na kupitia taasisi za kihaiti ili kutilia nguvu uwezo wao.Tusipo fanya hivyo tutakuwa tunazunguka kwenye mduara kwa miaka mingi ijayo.'

Wafadhili na washirika wengine wa kutoa misaada wamesisitiza kuwa nchi ya Haiti itapaswa kusimamia yenye ujenzi wake.Benki kuu ya dunia inatarajiwa kufanya kazi kama wakala wa mfuko wa wafadhili wa kimataifa utakaoundwa kwa ajili ya kuisaidia Haiti.


Mwandishi:Maryam Abdalla/Reuters.

Mhariri:Mohammed Abdulrahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW