1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haja ya hatua kali zaidi kukabiliana na itikadi kali

5 Juni 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May Jumapili(04.06.2017)  ametowa wito wa kuwapo kwa hatua kali zaidi kupambana na itikadi kali za Kiislamu kufuatia shambulio kwa kutumia gari na visu mjini London.

Britannien London - Terroranschlag
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Shambulio hilo lilianza na kumalizika haraka kwa polisi kuwauwa kwa kuwapiga risasi washambuliaji watatu katika muda usiozidi dakika nane.Lakini watu hao wametimiza lengo lao la kuugeuza usiku wa faraja mjini London kuwa wa balaa.

Shambulio hilo lilianza Jumamosi usiku wakati gari aina ya basi dogo lilipoacha njia na kungia katika njia ya wanaotembea kwa miguu katika daraja la London lenye harakati kubwa.Wanaume hao watatu walilikimbiza gari hilo wakiwa na visu vitatu vikubwa na kuwashambulia watu waliokuwa kwenye baa (vilabu vya pombe) na mikahawa karibu na soko la Borough kwa mujibu wa mashuhuda na polisi.

Maafisa wa huduma za dharura wamesema watu 48 wametibiwa katika hospitali za London wakiwemo wale waliokuwa na majeraha yenye kutishia uhai wao na wengine kadhaa waliokuwa hawakujeruhiwa sana. Idadi ya watu saba waliouwawa haijumuishi washambuliaji watatu.

Hilo ni shambulio la tatu kubwa kutokea nchini Uingereza katika kipindi cha miezi mitatu.Nchi hiyo tayari ilikuwa katika hali ya wasi kufuatia shambulio la bomu la kujitowa muhanga wiki mbili zilizopita katika onyesho la muziki wa Ariana Grande huko Manchester kaskazini magharibi mwa England ambalo limeuwa watu 22 na kujeruhi wengine wengi. Grande na wanamuziki wengine nyota Jumapili usiku walikuwa wakitarajiwa kupiga miziki wao katika onyesho la kuwachangia wahanga chini ya ulinzi mkali.

Itikadi kali yahusishwa

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.Picha: picture alliance/dpa/A.Matthews

Kundi linalojiita dola la Kiislamu limedai kuhusika na mpripuko wa bomu wa Manchester lakini bado hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo la London ambalo waziri mkuu amelihusisha na Uislamu wa itikadi kali.

May ambaye anakabiliwa na uchaguzi hapo Alhamisi amesema mashambulizi hayo ya hivi karibuni kabisa lilikiwemo lile lilitokea awali nje ya bunge hapo mwezi wa Machi hayahusiani moja kwa moja lakini "ugaidi huzaa ugaidi" na kwamba washambuliaji huwa wanaigizana . Amesema mashambulizi matano ya kuaminika yametibuliwa tokea mwezi wa Machi mwaka huu.

Amesema watu hao hunganishwa pamoja  na itikadi moja ya uovu itikadi kali ya Kiislamu ambayo huhubiri chuki, huchochea mgawanyiko na kuendeleza umadhehebu.

Amesema hiyo ni "itikadi inayodai kwamba maadili yetu ya kimagharibi na uhuru,demokrasia na haki za binaadamu hayaendani na dini ya Uislamu."

Kudhibiti mitandao

Maafisa wa polisi wakiwa kazini.Picha: Reuters/P.Nicholls

May ametowa wito kwa makampuni ya kimataifa ya mawasiliano kuchukuwa hatua zaidi za kuzuwiya makundi ya itikadi kali kujipenyeza kwenye mitandao ambayo wanaitumia kuwaandikisha wanachama kwa kutumia maandishi ya siri kuhusu njama.

Waziri Mkuu amesema uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.Vyama vikuu vilistisha kampeni za uchaguzi Jumapili kutowa heshima kwa wahanga juu ya kwamba chama cha UK Independence kimesema kitaendelea na kampeni kuwaonyesha watu wenye itikadi kali hawawezi kuikengeuka demokrasia.

Chama cha Conservative cha May kilikuwa kikitegemewa kupata ushubdi wa tofauti jubwa ya kura lakini uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni umeonyesha mchuano unazidi kuwa mkali.Haijulikani vipi matumizi hayo ya nguvu yasio kifani yanaweza kuwa na taathira kwa hisia za wapiga kura.

Mwandisi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri:Zainab Aziz

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW