Afrika yagawanyika juu ya waranti dhidi ya Bashir
5 Machi 2009Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu wa kivita ICC , ya mjini The Hague imepitisha uamuzi juu ya kutoa hati ya kisheria ya kuwezesha kukamatwa kwa rais Omar al Bashir wa Sudan.
Mahakama hiyo inadai kuwa rais huyo ametenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Lakini Afrika imegawanyika juu ya uamuzi wa mahakama hiyo.
Waafrika wengi wanaitilia mashaka mahakama hiyo ya kimataifa. Wanaona kuwa hadi sasa waliofikishwa mbele ya taasisi hiyo,hasa ni waafrika.Uchunguzi unafanyika katika nchi kadhaa za Afrika.
Rais wa tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping amesema kuwa siyo jambo la haki kwa mahakama ya ICC kuwafuatilia waafrika tu. Bwana Ping amesema inaonekana kana kwamba taasisi hiyo inafanya majaribio barani Afrika.
Nchi 53 za Afrika kwa kauli moja zimepinga waranti wa mahakama ya kimataifa dhidi ya rais al Bashir.Juu ya waranti huo waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernand Membe ameeleza kuwa, sasa itakuwa vigumu kuleta mchakato endelevu wa amani katika jimbo la Darfur, kwa sababu katika upande mmoja wanapelekwa wanajeshi alfu 17 wa kulinda amani katika jimbo hilo na katika upande mwingine harakati za kukamatwa rais Bashir zinasonga mbele.
Lakini katibu mkuu wa jumuiya ya wanasheria wa Afrika Moses Adriko amesema kuwa ,barani Afrika hakuna taasisi zinazofanya kazi zinazoweza kushughulikia uhalifu wa kiwango kikubwa kama huo.
Bwana Adriko pia amesema kuwa haoni sababu kwa nini kiongozi yeyote wa Afrika awe na wasi wasi ,ikiwa anafanya kazi yake kwa kutekeleza haki za binadamu na sheria za kimataifa nchi mwake.