1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria za viza zinayafungia mataifa maskini nje ya mikutano

6 Julai 2023

Sheria za mipaka na matakwa ya kusafiri nje ya nchi, zinawanyima wajumbe kutoka nchi maskini kuhudhuria mikutano na makongamano mengi ya kimataifa. Waandaji wahimizwa kuchagua nchi wenyeji zenye masharti nafuu ya visa.

Europa-Schengen-Visum im Reisepass
Picha: Nikolai Sorokin/Zoonar/picture alliance

Wakati wakili kutoka Nigeria Obioma Adesema Okonkwo alipopata mwaliko wa kuhutubia kongamano la kimataifa kuhusu haki za kidijitali nchini Costa Rica, alihakikisha amewasilisha ombi lake la visa miezi kadhaa kabla ya tarehe ya mkutano.

Kadri tarehe ilivyosogea bila jibu chanya, aliamua kuifutilia mbali safari hiyo na akawaarifu waandaaji wa kongamano hilo kuwa ataungana nao kwa njia ya mtandao.

Zaidi ya washiriki 300 hawakuweza kuhudhuria kongamano hilo kuhusu haki za kidijitali kwa sababu ya changamoto za kupata visa. Hayo yamesemwa na shirika la Access Now ambalo ndilo liliandaa kongamano hilo.

Nanjana Nyabola, Mkenya ambaye ni mwanachama wa bodi ya shirika hilo amesema kupitia ukurasa wa Twitter kwamba washiriki wengi Waafrika na kutoka bara Asia walikamatwa na maafisa wa mipakani wa Costa Rica na kushikiliwa kwa muda wa saa tatu. Wengine walirudishwa makwao moja kwa moja.

Wsshiriki wengi wa makongamano ya kimataifa wamekuwa wakinyimwa viza za baadhi ya mataifa wenyeji na hivyo kuwakosesha kushiriki mikutano ya kilele ya kimataifa.Picha: Fadel Senna/AFP

Shirika la kimataifa la Access Now lenye makao yake mjini New York, liliomba radhi kuhusu hayo yaliyotokea.

Ghadhabu kuhusu yaliyowakuta washiriki hao zimezusha mjadala kuhusu ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa visa, kati ya wajumbe wa mataifa tajiri na yale maskini wanapotaka kuhudhuria mikutano ya kimataifa.

Soma pia: Macron afungua mkutano wa kilele wa ufadhili wa fedha za hali ya hewa

Mikutano hiyo ya kimataifa hushughulikia masuala kama athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa mifumo ya kiuchumi na migogoro.

Washiriki kutoka nchi maskini hunyimwa viza

Okonkwo, ambaye ni afisa wa kisheria katika shirika la kutetea haki za vyombo vya habari Media Rights Agenda, amesema "ukiwa na kongamano la kimataifa, basi ni muhimu uzingatie kuna washiriki kutoka nchi maskini na ambao mara kwa mara hunyimwa Visa”.

Okonkwo amesema alitamani kujifunza mengi kutoka kwa wanasheria kutoka mabara mengine kwenye kongamano hilo. Lakini ndoto hiyo ilizimwa alipokosa kusafiri ili kushiriki vikao mbalimbali vya kongamano.

Nikki Gladstone, mkurugenzi wa shirika la RightsCon amesema waandaaji wa mikutano ya kimataifa wanapaswa kuhakikisha wawakilishi wamewasili na kwamba maoni yao ni muhimu.

Gladstone amesisitiza kuwa ni jukumu la waandaaji kujiandaa kwa changamoto hizo na wasaidie kuondoa vizingiti dhidi ya washiriki.

Serikali yaCosta Rica hata hivyo haikutoa jibu la moja kwa moja lilipoulizwa kutoa kauli.

Washiriki wakiwa katika kikao mojawapo cha Jukwaa la kimataifa la habari linaloandaliwa na DW.Picha: Florian Goerner/DW

Mwanaharakati wa mazingira kutoka Uganda Hamira Kobusingye asema kila mara anahitajika kuwasilisha nyaraka kadhaa anapotafuta visa ili kuhudhuria mikutano ya kimataifa.

Kitendo anachosema sivyo ilivyo kwa wajumbe wanaotoka nchi zilizoendelea.

Soma pia: Mkutano kuhusu uchumi wa Buluu wafanyika visiwani Zanzibar

Licha ya juhudi zake, alisema alinyimwa kibali cha kuhudhuria mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Bonn Ujerumani mwezi Juni mwaka huu na vilevile mkutano wa kimataifa kuhusu maji mjini New York.

Hali anayosema iliwakumba washiriki wengi kutoka barani Afrika. Amesema vizingiti hivyo huhujumu juhudi zao kama wanaharakati.

Afrika imeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi, mnamo wakati juhudi za kutafuta ufadhili wa kimataifa kukabili athari hizo katika mataifa maskini zikiendelea kudhoofika.

Kulingana na Kobusingye, yaonekana nchi tajiri za magharibi zinajaribu kutafuta suluhisho za tabia nchi bila kushirikisha sauti za watu wanaoathiriwa zaidi.

Na maadamu uwakilishi wao ni mkubwa kuliko wa nchi maskini kutokana na visiki vya vibali, wanaweza kuyashinikiza matakwa yao kwa urahisi.

Okonkwo na wanaharakati wengine wamependekeza pia kuwa mikutano hiyo ya kimataifa, iandaliwe katika nchi ambazo haziwabagui washiriki kutoka mataifa maskini kwa msingi wa vibali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW