1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za Binadamu Duniani na ripoti ya Amnesty International

Miraji Othman28 Mei 2008

Miaka 60 kuhusu haki za binadamu. Jee hakuna kitu zaidi ya hapo kilichopatikana? Kweli, vipimo vingi kuhusu haki za binadamu vimewekwa, tena kwa njia nzuri.

Nembo ya Shirika la Amnesty International la kupigania haki za binadamu duniani

Hivyo ndivyo linavosema shirika kubwa lisilokuwa la kiserekali linalotetea haki za binadamu duniani, Amnesty International, katika ripoti yake ya mwaka huu. Lakini vipi hali halisi ya mambo ilivyo? Vipi serekali zinatekeleza ahadi ilizotoa tangu miaka 60 iliopita za kuufuata ule muongozo unaotaka zihakikishe kwamba raia wao wanapata usawa, haki, utawala wa sheria na heshima ya kiutu?

Pale Shirika la Amnesty International linaposema kwamba katika mwaka uliopita, peke yake katika nchi 181 duniani, watu waliteswa na kutendewa mambo yasiokuwa ya heshima na uutu, basi hiyo peke yake ni picha inayotisha. Pale magazeti na uhuru wa watu kutoa maoni yao unakanyagwa kabisa katika nchi hizo, basi mtu anakaribia kufikia uamuzi kwamba viongozi wa kisiasa walio na dhamana katika nchi hizo wanataka tu kuhakikisha wana'gan'gania madaraka yao kwa njia ya ujangili na wanakubali kuachana na utamaduni wa kidemokrasia. Pale katika nchi kadhaa wanapodharauliwa na kubaguliwa wanawake, hasa tu kwa sababu ya jinsia yao, basi huo sio tu ni ushahidi wa kukosekana usawa, lakini ni kuweko msingi wa mfumo dume unaojinata.


Duniani kote raia wanataka serekali zenye kutenda mambo kwa ukweli, serekali zilizo tayari kubeba dhamana na zilizopata imani ya wananchi. Tena serikali hizo ziwe tayari kushindana kwa misingi ya kidemokrasia kufikia uvumbuzi unaowezekana kabisa wa matatizo, kwa maslahi ya wananchi. Na tusisahau kwamba utanda wazi umewaweka wanadamu mbele ya mitihani mipya. Mabadiliko ya hali ya hewa na maafa ya kimaumbile, kupotea viumbe na mimea na maishaanuai, hivyo kupotelewa na misingi ya maisha, umaskini unaozidi, maradhi ya Ukimwi na Malaria, hayo ni machache kati ya mitihani hiyo. Mitihani hiyo kuikiuka kwa njia ya kushauriana na kuachana na mtindo wa kulinda tu maslahi mwishowe ndio yawe malengo ya serekali zote- bila ya kujali kama serekali hizo ziko Myanmar au Zimbabwe, Pakistan au Sudan, Iraq au Afghanistan.


Pia nchi hizo bila ya shaka ni rahisi kwao kuchukuwa jukumu hilo la kuheshimu haki za binadamu pale dola zinazodai kutaka kuongoza dunia, kama vile Marekani, zinapoachana kusema kwa ndimi mbili, kama zilivojionesha hivi karibuni. Pale watu, bila ya mashtaka na bila ya kufikishwa mahakamani, wanaendelea kuwekwa vizuizini, kama kule Guantenamo, au pale shirika la ujasusi la Kimarekani, CIA, linaruhusu kutumia mitindo ya kutesa watu kwa kuwadidimiza vichwa vyao katika maji kwa muda mrefu, basi nchi hizo zinakuwa haziaminiki, na hasa pale zinapojaribu kuwakaripia wengine na kuwataka waheshimu haki za binadamu.


Lakini pia nchi kama vile China na Russia lazima zitanzuwe matatizo yao makubwa kuhusu kuheshimiwa haki za binadamu ndani ya nchi zao.


Pia mfumo unaosifiwa duniani wa kuheshimiwa haki za binadamu katika nchi za Umoja wa Ulaya unahitaji kuwa wazi kutokana na mitihani mipya. Kwa mujibu wa Shirika la Amnesty International ni kwamba hakuna serekali ya nchi ya Umoja wa Ulaya ilioonesha kwamba siku za mbele haitashiriki katika utekeaji nyara wa kisirisiri unaofanywa na idara za kijasusi za Marekani.


Hata hivyo, Tangazo la kimataifa la kuheshimiwa haki za binadamu ambalo sasa ni miaka 60 tangu litolewe ni tarajio na pia ahadi kutokana na dhuluma zilizokuwa zikifanyika mamia ya miaka iliopita. Ripoti ya mwaka ya Amnesty International ni ushahidi kwamba jumuiya ya kiraia ilio na machachari inaweza kwa utahbiti ikashikilia kwamba duniani kote zitekeklezwe zile ahadi zilizotolewa na mataifa.