1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za wakimbizi bado zakiukwa

Gregoire Nijimbere16 Juni 2005

Kulingana na ripoti ya shirika la kimarekani la Kamati kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji USCRI, asili mia 70 ya wakimbizi duniani, wamekaa kwa miaka kadhaa katika nchi ambako haki zao za kimsingi zinakiukwa.

Kambi ya wakimbizi nchini Syria
Kambi ya wakimbizi nchini SyriaPicha: AP

Ripoti hiyo ya mwaka wa 2005, imetolewa katika kampeni ya shirika hilo la kimarekani la kupigania haki za wakimbizi na imechapishwa kwa kuzingatia hali ya mambo katika nchi 40.

Marekani iko mbele pamoja na Iraq na Chad, kwenye orodha ya nchi ambazo zinakiuka haki za wakimbizi.

Tanzania, Malaysia na Iran, zimewekwa miongoni mwa nchi ambazo haziheshimu haki za wakimbizi.

Fani nne muhimu ndizo zilizingatiwa katika kuchapisha ripoti hiyo. Hizo ni pamoja na namna serikali zinazozingatia utaratibu wa kuwapokea na kuwalinda wasirudishwe nyuma kwa mfano au wasihamishwi kwa nguvu.

Pia kama wakimbizi wamefungwa na katika mazingira gani.

Halafu kama wakimbizi hao wanalo pato linalodhaminia maisha yao, kumiliki mali na kuweza kupata kazi kulingana na sheria.

Hatimae kama wakimbizi hao wanao uhuru wa kutembea ndani na nje ya nchi walikokimbilia.

Nchi kama Marekani, Tailand, Pakistan, Rushia, na Lebanon ziko kwenye msitali wa mbele wa nchi ambako mkimbizi anakabiliwa na hatari ya kurudishwa hata kwa nguvu katika nchi alikotoka. Lakini kuhusu kudhaminia haki ya pato la kuwawezesha kuishi, Marekani inaongoza vizuri.

Kulingana na ripoti hiyo ya Kamati kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, katika nchi ambako huduma hizo nne muhimu hazidhaminiwi kama unavyoagiza mkataba wa kimataifa wa mjini Geneva kuhusu wakimbizi, matokeo yake ni kwamba wakimbizi wengi hawana kazi, hawawezi kutembea watakavyo, hawamiliki chochote na wanakosa elimu na kadhalika.

Hata hivyo, shirika hilo, limekiri kuwa idadi ya wakimbizi duniani imepungua kidogo kutoka milioni 11,9 mwaka jana hadi milioni 11,5 mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa jumla idadi hiyo imeendelea kupungua ukulinganisha na mwaka wa 1996 ambapo walikuwa milioni 14,5.

Kupungua kwa idadi ya wakimbizi mwaka jana, kulitokana na kurejea nyumbani kwa wakimbizi laki 4 kutoka Afghanistani, laki1 kutoka Angola, 75 elfu kutoka Eritrea na 60 elfu kutoka Liberia. Idadi hiyo ni zaidi ya yile ya wakimbizi wapya laki 1 kutoka Sudan na wengine kama 80 elfu kutoka Myammar, Burundi na Iraq.

Hata idadi ya wakimbizi wa ndani imeshuka kiasi kutoka milioni 23,6 mwaka wa 2003 hadi milioni 21,6 mwezi Januari mwaka huu. Sawa na kupungua kwa milioni 3.

Hali hiyo imetokana na kuwa maelfu ya waliolazimishwa na vita kuyahama maskani yao katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Angola walirudi nyumbani, japokuwa nchini Sudan waliongezeka kutokana na vita katika jimbo la magharibi la Darfur ambako zaidi milioni 2 waliyahama makaazi yao.

Wakimbizi wa kipalestina ndiwo wa tangu jadi kuliko wakimbizi wengi. Takriban wapalestina milioni 3 wanaishi katika nchi zingine za kiarabu kwa zaidi ya nusu karne.

Idadi inaokisiwa kufika milioni 1 na laki ni wakimbizi wa ndani katika maeneo yao ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW