Hakuna aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Ukraine
8 Januari 2020Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema hakuna mtu aliyesalimika katika ajali hiyo iliyotokea leo asubuhi. Zelensky amesema amesikitishwa na ajali hiyo na ametuma salamu za pole kwa ndugu na marafiki wa abiria wote pamoja na wafanyakazi wa ndege hiyo. Zelensky amesema Ukraine inachunguza mazingira yaliyosababisha ajali hiyo pamoja na vifo.
Kutokana na ajali hiyo, Zelensky amekatisha ziara yake nchini Oman na kurejea Kiev. Rais huyo amesema Ukraine imetoa ndege maalum ambayo iko tayari kwenda Iran kuichukua miili ya waliokufa katika ajali hiyo, japokuwa wanasubiri makubaliano kutoka Iran.
Aidha, Zelensky ameonya kuhusu uvumi juu ya ajali ya ndege na amewataka watu kutobashiri chochote na kuweka nadharia zisizo na uthibitisho.
Televisheni ya taifa ya Iran na Waziri Mkuu wa Ukraine, Oleksiy Honcharuk wamesema abiria 167 na wafanyakazi 9 walikuwemo ndani ya ndege hiyo wamefariki. Kwa mujibu wa televisheni ya Iran, abiria 32 walikuwa raia wa kigeni kutoka Iran, Canada na Sweden.
Vyombo vya habari vya Iran vimemnukuu afisa wa mamlaka ya anga wa Iran akisema kuwa rubani wa ndege hiyo hakutoa tahadhari yoyote ya kuwepo hali ya dharura.
Kwa mujibu wa televisheni ya Iran, moja ya visanduku viwili vya kunakili kumbukumbu ya mawasiliano ya ndege kimepatikana na kwamba ajali hiyo imesababishwa na matatizo ya kiufundi, ingawa haikutoa taarifa zaidi.
Pirhossein Kulivand, mkuu wa idara ya dharura ya Iran amesema wafanyakazi wa uokozi wanaendelea na shughuli za kuiondoa miili katika eneo la ajali.
''Moto umezimwa kabisa. Tuko kwenye eneo la ajali. Tumeziarifu kampuni za mazishi na zile zinazochunguza vifo vya ghafla kuleta magari yao ya kubeba wagonjwa haraka iwezekanavyo, ili miili ipelekwa kwenye maeneo maalum kwa ajili ya kuitambuliwa na kufanyiwa uchunguzi,'' alifafanua Kulivand.
Shirika la Hilal Nyekundu limesema ndege hiyo ya shirika la kimataifa la ndege la Ukraine, ilikuwa ikisafiri kutoka Tehran kwenda Kiev na iliondoka majira ya saa kumi na moja asubuhi kwa saa za Iran. Ndege hiyo ilianguka na kuwaka moto katika kitongoji cha Parand.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani, FAA imezipiga marufuku ndege za kibiashara kuingia kwenye anga ya Iran, Iraq na Ghuba ya Uajemi, baada ya Iran kuzishambulia kambi mbili za jeshi la Marekani nchini Iraq.
Mashirika kadhaa ya ndege yamebadilisha njia ya ndege zake katika anga ya Mashariki ya Kati kutokana na kuongezeka wasiwasi wa mvutano kati ya Marekani na Iran. Mashirika hayo ni pamoja na ya Australia, Malaysia na Singapore.
(AFP, DPA, AP, Reuters)