1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna maafikiano kuhusu makaazi ya walowezi wa Kiyahudi

16 Septemba 2010

Majadiliano ya amani ya Mashariki ya Kati yamemalizika bila ya makubaliano kupatikana kuhusu mada tete kabisa ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi iliyokaliwa katika Ukingo wa Magharibi.

Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu shakes hands with Palestinian president Mahmoud Abbas, at his residence in Jerusalem, Israel Wednesday, Sept. 15, 2010. Clinton is in the region for Mideast peace talks. U.S. Secretary of State Hillary Rodham Clinton on Wednesday said Israeli and Palestinian leaders are "getting down to business" on core issues of renewed peace talks, but gave no sign they are any closer to resolving a looming crisis over Israeli West Bank settlements. (AP Photo/Alex Brandon, Pool)
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu(kushoto) na Rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas walipokuta Jerusalem,15 Septemba 2010.Picha: AP

Ujenzi wa makaazi hayo ya walowezi wa Kiyahudi ni miongoni mwa mada kuu zilizoshughulikiwa katika majadiliano yaliyofanywa kati ya Netanyahu na Abbas chini ya uongozi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton. Rais Abbas ameonya kuwa atajitoa kwenye majadiliano hayo ya ana kwa ana ikiwa muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi hayo unaomalizika mwisho wa mwezi huu hautorefushwa. Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu Netanyahu amekataa kurefusha muda huo. Lakini baada ya kushinikizwa na Rais wa Marekani Barack Obama kurefusha muda huo, Netanyahu ameashiria kuwa yeye atachukua hatua za kudhibiti ujenzi wa makaazi hayo katika Ukingo wa Magharibi.

George Mitchell, mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati.Picha: AP

Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell, amesema mazungumzo hayo ya siku mbili yalikuwa ya dhati na ya maana.Ameeleza hivi:

"Ningesema kuwa viongozi hao wawili hawayaachilii masuala magumu hadi mwisho wa majadiliano yao. Tangu mwanzo wameshughulikia masuala hayo yaliyo kiini cha mzozo wa Waisraeli na Wapalestina."

Kwa maoni ya Mitchel, hiyo ni ishara dhahiri kuwa viongozi hao wanaamini kuwa amani inaweza kupatikana na kwamba wamedhamiria kupata makubaliano. Na hiyo anasema, inatia moyo. Clinton nae amesema, wakati ni huu na viongozi ni hao. Marekani itasimama bega kwa bega na viongozi hao watakapopitisha maamuzi magumu.

Mwanzoni mwa mkutano wa pande tatu, Netanyahu alisema kuwa kuna kazi nyingi za kufanywa na amefurahi kupata nafasi ya kuwakaribisha Rais Abbas na waziri wa nje Clinton katika jitahada za kupata amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton akiwapungia mkono waandishi wa habari baada ya kukutana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas,mjini Ramallah 16 Septemba 2010.Picha: AP

Hii leo Hillary Clinton akijitahidi kuyaendeleza majadiliano hayo ya ana kwa ana yaliyoanzishwa hivi karibuni, amekutana tena na Rais Abbas mjini Ramallah. Baadae hii leo atakutana na Mfalme Abdallah wa Jordan mjini Amman. Wakati huo huo, George Mitchell atakuwa na majadiliano pamoja na Rais wa Syria Bashar al-Assad mjini Damascus katika jitahada ya kuyafufua majadiliano ya amani kati ya Syria na Israel.

Muandishi: Martin,Prema/DPAE/APE

Mpitiaji: Othman, Miraji