Hakuna makubaliano kati ya Ugiriki na Umoja wa Ulaya
17 Februari 2015Ugiriki imekataa ushauri wa Umoja wa Ulaya wa kuurefusha mpango wa uokozi ambao muda wake utakamilika mwishoni mwa mwezi huu. Baada ya mkutano ambao haukuchukua zaidi ya saa tatu, waziri wa fedha wa Ugiriki, Yanis Varoufakis, aliondoka Brussels mikono mitupu: Alikuwa anaamini kwamba atafanikiwa kuwashawishi mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro, wakubali pendekezo lake la mpango mbadala wa kubana matumizi. Ni jambo ambalo mawaziri walilikataa.
Mkuu wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Jeroen Dijsselbloem, hata hivyo anataka kuipa Ugiriki nafasi nyingine kuweka mambo yake sawa. "Tulikuwa na mazungumzo kuhusu hatua za kuchukua na sisi wa nchi zinazotumia Euro tunaamini kwamba njia bora zaidi ni Ugiriki kuomba mpango wa kubana matumizi urefushwe," amesema Dijsselbloem. "Hii itatupa muda wa miezi kadhaa kuweka mipango zaidi."
Athens kuwasilisha mapendekezo mapya
Ugiriki sasa imepewa muda hadi mwishoni mwa wiki hii kuamua kama inataka kurefusha mpango uliopo au la. Umoja wa Ulaya mpaka sasa umeonyesha kuwa hauko tayari kupokea pendekezo lingine. Hata hivyo Umoja huo umeahidi kwamba Ugiriki itaruhusiwa kuufanyia mpango uliopo marekebisho kidogo, lakini bila kutumia kiasi kikubwa cha fedha kitakachopindukia kiwango ambacho Umoja wa Ulaya umeruhusu. Pamoja na hayo waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras lazima ashauriane na wakopeshaji wake ambao ni Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha Duniani IMF na Benki Kuu ya Dunia iwapo atataka kufanya mabadiliko yoyote kwenye mfumo wa ushuru, sera za ajira na pia ubinafsishaji.
Yanis Varoufakis amesema hakufurahishwa kabisa na yaliyojiri kwenye mkutano wa Brussels. "Mkutano huu umedhihirisha kwamba Ulaya inapata wakati mgumu kukubali kuwa Ugiriki sasa ina serikali mpya, serikali inayoshuku huu mpango wa kubana matumizi ambao umekuwepo kwa miaka mitano na ambao umeshindwa kutimiza malengo yake," amesema waziri huyo. "Sisi tuna kibarua cha kuwashawishi washirika wetu kwamba lazima waachane na huu mpango usiofanya kazi."
Hata kabla ya mkutano wa Jumatatu kuanza, wajumbe hawakuonyesha matumaini kwamba kutakuwa na mafanikio yoyote. Pande zote mbili hazikuwa tayari kubadili mawazo. Hakuna tarehe iliyowekwa kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo. Hata hivyo wizara ya fedha ya Ugiriki mara baada ya mkutano ilitoa tamko linalosema watafanya kila liwezekanalo kufikia makubaliano na Umoja wa Ulaya ndani ya siku mbili.
Mwandishi: Barbara Wesel
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Hamidou Oummilkheir