1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna msaada bila ya demokrasia, Marekani yaiambia Sudan

23 Novemba 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewaambia viongozi nchini Sudan kwamba nchi hiyo inahitaji kupiga hatua zaidi katika demokrasia kabla ya Marekani kurejesha tena msaada wa dola milioni 700 uliositishwa

Antony  Blinken
Picha: Andrew Harnik/Pool/AP/picture alliance

 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, hapo jana aliwaambia wanahabari kwamba hatua ya Blinken ya kuzungumza na viongozi hao siku moja baada ya waziri huyo mkuu aliyepinduliwa Abdalla Hamdok kurejeshwa madarakani ni hatua ya mwanzo na wala sio ya mwisho. Price ameongeza kuwa msaada haujaanza kutolewa na kwamba maamuzi hayo yatategemea kitakachotokea katika masaa, siku ama wiki zijazo:

Ned amesema kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, alipata fursa ya kuzungumza na Waziri Mkuu Hamdok na pia Jenerali al-Burhan na kwa msingi huu ujumbe uliokuwa wazi ni kwamba lazima maendeleo yaonekane na Sudan kuonekana kurudi  kwenye njia ya kidemokrasia na hiyo inaanza na kurejeshwa madarakani kwa waziri mkuu lakini  hakika haishii hapo.

Sudan iliingia katika mpango dhaifu wa kugawana madaraka kati ya wanajeshi na raia baada ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais Omar al-Bashir mnamo mwaka 2019, huku uchaguzi ukitarajiwa mwaka 2024.
Kutokana na hilo,  Marekani ilijitolea kuunga mkono kipindi hicho cha mpito kupitia mfuko wa msaada wa dola milioni 700, ambao iliusimamisha wakati Burhan alipomuondoa madarakani Hamdok na baadaye kuwateua wanachama wapya wa baraza tawala.

Abdel Fattah al-Burhan - Kiongozi wa jeshi nchini SudanPicha: Sudan TV/AP/picture alliance

Wakati huo huo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al-Jazeera yaliyorushwa hapo jana, Hamdok alisema kuwa atakuwa na mamlaka ya kuunda serikali yake huru kulingana na makubaliano aliyotia saini siku ya Jumapili na viongozi wakuu wa jeshi nchini humo na kwamba anaona serikali ijayo ikilenga zaidi kuandika upya katiba ya nchi hiyo na kuandaa uchaguzi kwa wakati.

Mamlaka nchini Sudan pia imewaachia huru viongozi wa kiraia waliokuwa wamezuiwa tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita. Haya yamesemwa jana na Omar al-Degeir, kiongozi wa chama cha Congress nchini humo ambaye pia aliachiwa huru. Wanasiasa wengine wa kiraia walioachiliwa huru ni Sedeeq al-Sadiq al-Mahdi wa chama cha Umma ambacho ni chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini Sudan. Hata hivyo, chama cha Congress kimeyapinga makubaliano Jumapili kati ya watawala wa kijeshi na Abdalla Hamdok na kusema yalihalalisha wazi kuendelea kwa utawala wa mapinduzi.