Mwamko mpya wakosekana Zimbabwe baada ya uchaguzi
7 Agosti 2018Wazimbabwe walikuwa na nafasi ya kipekee katika uchaguzi wa kihistoria ambao ni wa kwanza kufanyika bila Robert Mugabe aliyetawala taifa hilo kwa mkono wa chuma kwa karibu miaka 40. Hata hivyo wachambuzi wanasema ushindi wa rais aliyeko madarakani Emmerson Mnagagwa hauonekani kuleta mabadiliko zaidi yanayohitajika kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Muda mfupi tu baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Mnangagwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 50.8 ya kura mitaa ya mji mkuu Harare ilishuhudiwa kuwa kimya badala ya kuonesha matumani kwa matarajio ya maisha bora katika siku zijazo.
"Licha ya kuondolewa kwa Mugabe katika uongozi wa nchi hiyo lakini bado hali inaonekana kuwa ileile hasa linapokuja suala la siasa," anasema Charles Laurie ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kiusalama.
Wakati Mnangagwa alipomuengua madarakani Robert Mugabe kupitia mapinduzi ya amani yaliyofanywa na jeshi mwishoni mwa mwaka 2017 matarajio yalikuwa makubwa kuwa demokrasia itarejea katika taifa hilo lenye watu karibu ya milioni 16. Hata hivyo matumaini hayo yalianza kutoweka wakati wa kipindi cha kampeni ambacho kilishuhudiwa Mnangagwa na chama chake tawala cha ZANU-PF kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Mugabe akirejea madakani akitumia taasisi za serikali pamoja na vyombo vya habari .
"Hali ya kuchanganyikiwa kwa watu inaeleweka vema, kwa sabababu kwa wakati fulani kampeni hazikufanyika katika mazingira yaliyo huru na haki kwa vyama vyote, vyombo vya habari vya serikali vilionekana kupendelea na pia watu walitishwa hususani katika maeneo ya vijijini na katika hali fulani walilazimishwa kumpigia kura Mnangagwa" amesikika Nobert Neuser, mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya unaohusika na masuala ya bunge, alipozungumza na shirika la habari la dpa.
Neuser anaongeza kuwa watu ambao uchaguzi huu ulikuwa ni hatua muhimu kwao kisiasa wanahisi kuwa wamedanganywa.
Upinzani wayakataa matokeo
Mgombea wa upinzani Nelson Chamisa aliyeshindwa uchaguzi baada ya kupata asilimia 44.3 ya kura ametangaza kuyakataa matokeo akidai udanganyifu na kuwa uchaguzi huo haukuwa halali.
Chamisa ameapa kupinga matokeo hayo lakini hata hivyo wachambuzi wanaamni kuwa hatua hiyo itakuwa ngumu kwa mgombea huyo mwenye umri wa miaka 40 pamoja na chama chake cha Movement for Democratic Change -MDC kulifikisha suala hilo mahakamani.
"Hatujaona ushahidi ambao utakipa nguvu kisheria chama cha MDC kupinga matokeo hayo mahakamani," anasema Derek Matyszak, mchambuzi wa taasisi inayohusika na masuala ya usalama katika kanda ya Afrika, alipozungumza na shirika la habari la dpa mjini Harare.
Kwa upande mwingine ukiacha hilo wachambuzi wanasema mawakala wa vyama vyote wamesaini fomu za matokeo ya uchaguzi katika vituo vyote vya kupigia kura nchini humo, hali inayofanya hatua ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani kuzidi kuwa ngumu.
Aidha ushindi mwembamba aliopta Mnangagwa unampa changamoto kubwa kuongoza kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura kugawanyika hivyo kutakiwa kuanza kuwajumuisha asilimia 50 ya wale ambao hawakumpigia kura ili kuthibitisha kuwa ataongoza kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.
Hayo yanajiri mnamo wakati wanachama 24 wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe (MDC) wakifikishwa mahakamani wakituhumiwa kufanya vurugu ikiwa ni baada ya rais Emmerson Mnangagwa wa chama tawala ZANU-PF kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Jumatatu.
Wanachama hao wanadaiwa kufanya vurugu katika ofisi za chama tawala pamoja na kuchoma moto magari. Kiasi watu sita walifariki dunia baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji hatua iliyokumbusha kumbukumbu ya vurugu baada ya uchaguzi wakati wa utawala wa Robert Mugabe.
Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/ECA
Mhariri: Sekione Kitojo