Tanzania yaanza kurejea hali ya kawaida baada ya uchaguzi
4 Novemba 2025
Wananchi wameanza kuonekana wakitembea mitaani ikiwa siku moja tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa kwa muhula wake wa pili na kuamuru raia warejea katika maisha yao ya kawaida.
Huduma kama intaneti, usafiri binafsi na ule wa umma, biashara ndogondogo zinarejea taratibu katika maeneo mengi ya nchi hasa yale yaliyoshudia vurugu na maandamano wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 na kisha kufuatiwa na hali ya sintofahamu.
Intaneti bado ni ya kusuasua
Lakini hata hivyo upatikanaji wa baadhi ya huduma hizo bado siyo wa kuridhishwa ikiwamo intaneti iliyorejeshwa jana jioni lakini kuanzia leo asubuhi mitandao mingi iko katika kiwango cha chini.
Utumaji na upakuaji wa vidio pamoja na picha mnato uko katika kasi ya chini huku baadhi ya watumiaji wake wakikata tamaa kutokana na kushindwa kufanya biashara zao zinazotegemea mtandao ambao ulikatwa tangu Oktoba 29 siku ambayo Watanzania walikuwa wakipiga kura.
Ingawa mamlaka zimeruhusu shughuli zote kurejea katika hali ya kawaida, huko mitaani bado kunashuhudiwa hali ya wasiwasi na maduka mengi ikiwamo yale yanayouza vyakula yameendelea kufungwa. Lakini tatizo la ukosefu wa mafuta kutokana na vituo vingi kufungwa sasa limeanza kupungua na amri ya kubakia ndani baada ya saa 12.00 za jioni bado ingali kwenye akili za wengi, na bado wana hofu.
Mamlaka bado ziko kimya juu ya taarifa za vifo vya waandamanaji
Kumekuwa na ripoti juu ya vifo vingi, lakini hadi sasa mamlaka bado haijataja idadi jumla lakini mashirika ya kiraia pamoja na wachunguzi wa mambo wanasema idadi ya watu waliopoteza maisha imepindukia ile iliyoripotiwa katika vurumai za wakati wa uchaguzi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992.
Wiki iliyopita chama cha upinzani CHADEMA kilisema watu wasiopungua 700 waliuawa katika siku tatu za baada ya uchaguzi, taarifa ambazo zilikanushwa vikali na serikali ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan kesho Jumatano anatarajiwa kumwapisha mwanasheria mkuu wa serikali Hamza Johari aliyemrejesha kwenye nafasi yake. Taarifa ya Ikulu imesema mtendaji huyo ataapishwa kesho huko Chamwino, Dodoma.