1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali inatisha nchini Gabon

Oumilkher Hamidou1 Septemba 2009

Wagombea watatu wajitangazia ushindi hata kabla ya matokeo kutolewa

Rais wa zamani wa Gabon marehemu Omar BongoPicha: picture-alliance/ dpa

Hali ni tete kabisa hii leo mjini Libreville,mji mkuu wa Gabon,ambako matokeo ya uchaguzi wa rais ulioitishwa jumapili iliyopita,yanatarajiwa kesho huku wagombea watatu,Ali Bongo.André Mba Obame na Pierre Mamboundou ,kila mmoja akidai ameshinda.

Pirika pirika za usafiri ambazo kawaida huhanikiza,zimepwaya hii leo mjini Libreville ambako vikosi vya usalama vimetawanywa katika maeneo muhimu na karibu na njia panda za mji huo.

"Watu wanaogopa ndio maana wameamua kusalia majumbani mwao" amesema dereva mmoja wa taxi ambae mwenyewe anaonyesha kua na hofu.

Wananchi wengi wa Gabon wanahofia pasije pakatokea fujo baada ya uchaguzi wa jumapili ambao wagombea watatu wakuu,wanadai wameibuka na ushindi.

Idadi ya walioteremka vituoni haijulikani na matokeo ya mwanzo pia bado hayajatangazwa.Kamisheni huru na ya kudumu ya uchaguzi-Cénap-imesema matokeo yatatangazwa kesho usiku.

Tangu jumapili usiku,wagombea watatu wa kiti cha rais wamekua wakibishana kupitia njia zote za mawasiliano zilizopo.

Jana usiku kambi ya waziri wa zamani wa mambo ya ndani André Mba Obame,imetuma risala ya SMS,ikihoji wamejikingia asili mia 50.1 ya kura,katika wakati ambapo siku moja kabla kambi ya kiongozi mashuhuri wa upinzani Pierre Mamboundou imesema katika mkutano pamoja na waandishi habari mgombea wao ameibuka na ushindi kwa asili mia 39.15 ya kura.Mapema jana,mtoto wa marehemu Omar Bongo,Ali Bongo alisema pia ameshinda "kwa wingi wa kura."

Katika makao makuu ya chama cha Muungano kwaajili ya mageuzi na nidhamu-ACR-muungano wa vyama vitano vinavyo muunga mkono Pierre Mamboundou,hali inatisha hii leo.Mamia ya wafuasi wake wamelala mbele ya makao makuu hayo,wakihoji "wamekusanyika ili kuuhami ushindi wao,kuwalinda viongozi wao na kuhifadhi nyaraka za vituo vya upigaji kura."

"Viongozi wakimtangaza Ali Bongo kua ndie mshindi wa uchaguzi na kutuma wanajeshi,basi tutageuka sisi kua wanajeshi na wao raia.Wananchi wataibuka na ushindi na mgombea wa chama tawala cha PDG ataihama Gabon." ametishia mwanachama mmoja wa chama cha ACR.

Wafuasi wa waziri wa zamani wa mambo ya ndani Mba Obame aliye onya dhidi ya kile alichokiita "kupinduliwa matokeo ya uchaguzi",nao pia wamechukua hatua kama hizo na kupiga kambi mbele ya nyumba ya mgombea wao karibu na uwanja wa ndege-kaskazini magharibi ya Libreville.

Wafuasi wa Ali BongoPicha: AP

Katika wakati ambapo wagombea hao watatu wanadai wameshinda,mgombea wa kwanza wa kike Victoire Lasséni Duboze amekiri ameshindwa.

Amewatolea mwito wananchi wa Gabon waondowe hofu walizo nazo.

Katika mahojiano pamoja na gazeti la "Le Parisien" katibu wa dola wa Ufaransa anaeshughulikia masuala ya ushirikiano,Alain Joyandet amesema"rais mpya wa Gabon atabidi abadilishe mambo ili kugawa kwa njia ya haki utajiri wa nchi hiyo miongoni mwa jamii."

Amehakikisha kwa mara nyengine tena Ufaransa haimpendelei mgombea yeyote yule.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(AFP)

Mhariri:Abdul Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW