Hali inatisha nchini Syria,asema Lakhdar Brahimi
5 Septemba 2012Katika wakati ambapo mzozo wa Syria unaingia katika mwezi wa 18,bila ya kuwepo matumaini ya kuupatia ufumbuzi,matumizi ya nguvu yanazidi makali-pekee hii leo watu wasiopungua 20 wameuwawa jeshi la serikali lilipouhujumu mji wa Aleppo,walikopiga kambi waasi,zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Katika hotuba yake ya kwanza mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York,tangu alipoanza rasmi shughuli zake kama mpatanishi wa mzozo wa Syria,Lakhdar Brahimi amezungumzia ziara anazopanga kufanya hivi karibuni mijini Damascus na Cairo.-
Anahisi ni muhimu kupata uungaji mkono wa jumuia ya kimataifa ambayo haina msimamo mmoja linapohusika suala la namna ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa Syria;warusi,wachina na wairan-washirika wa utawala wa Bashar al Assad wakipinga mpango wowote wa kuingiliwa mzozo huo na mataifa ya kigeni ,huku nchi za magharibi na washirika wao wa kiarabu wakiwaunga mkono waasi.
"Idadi ya wahanga inamfanya mtu aduwae,hali inazidi kuwa mbaya" ameonya mwanadiplomasia huyo aliyeshika nafasi iliyoachwa na Kofi Annan na kufafanua umuhimu wa ushirikiano wa jumuia ya kimataifa.Bwana Lkhdar Brahimi ameongeza kusema:"Mustakbal wa Syria utaamuliwa na wananchi wake wenyewe na sio na wengine.Uungaji mkonmo wa jumuia ya kimataifa ni jambo la lazima na linalohitajika haraka.Uungaji mkono huo utaleta tija tu ikiwa wote watakuwa na msimamo mmoja."
Nae katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,akihutubia pia mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New York,amezikosoa nchi zinazozipatia silaha pande zinazohasimiana nchini Syria. na kutoa mwito wa kuwepo mshikamano wa jumuia ya kimataifa ili kuwapatia huduma za kiutu wakimbizi wa Syria ndani na nje ya nchi hiyo.
Urusi na Iran zinatuhumiwa kuupatia silaha utawala wa Bashar al Assad huku Saud Arabia na Qatar zikitajwa kuwapatia silaha waasi.
Mjini Berlin waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle,amezungumzia "umuhimu wa kuundwa serikali ya mpito ya kidemokrasi itakayoundwa na pande zote zinazoupinga utawala wa Bashar al Assad."Matamshi hayo ameyatoa mwito mwa mkutano wa Marafiki wa Syria uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zisizopungua 60 mjini Berlin.
Wakati huo, huo mkuu wa shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu anaendelea na ziara yake nchini Syria.Msemaji wa shirika hilo Rabab Rafai amezungumzia "mazungumzo ya maana" aliyokuwa nayo bwana Peter Mauer na rais Assad.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri Yusuf Saumu