Baa la njaa lakithiri Sudan Kusini
6 Novemba 2015Mwezi uliopita mashirika ya Umoja wa Mataifa yalieleza kwamba watu 30,000 wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa katika jimbo la Unity huku wataalamu hao wa kitengo maalum kinachoshughulikia suala la usalama wa chakula IPC wakitahadharisha kwamba kuna hatari kubwa ya kuzuka kwa ukame kabla ya mwishoni mwa mwaka huu ikiwa mapigano yataendelea na msaada kushindwa kuyafikia maeneo yaliyoathirika vibaya.Licha ya tahadhari hiyo sambamba na kutiwa saini makubaliano ya amani mnamo mwezi Agosti bado vikosi vya serikali vinapambana na waasi nchini humo huku wanadiplomasia wazilaumu pande zote mbili kuhusika na matukio ya kuzuia msaada wa kuokoa maisha ya raia.
Shirika ,la madaktari wasiokuwa na mipaka MSF limeonya kwamba mgogoro wa kibinadamu kusini mwa jimbo la Unity umefikia kiwango cha kutisha huku yakishuhudiwa mapambano ya mara kwa mara yanayowalenga pia raia wasiokuwa na hatia.Shirika hilo lililojipatia sifa ya kuendesha shughuli zake hata katika sehemu hatari kabisa duniani ambako kuna mapigano limesema halijawahi kushuhudia kiwango cha vurugu na unyama kama inaoushuhudia nchini Sudan Kusini.
Katika wakati ambapo bado haijatangazwa rasmi kuwepo baa la njaa nchini Sudan Kusini ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inazungumzia kuwepo hali mbaya kabisa ambayo haijawahi kuonekana katika takriban miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambavyo vimetawaliwa na mauaji ya kinyama ya watu wengi pamoja na madai ya uhalifu wa kivita ikiwemo ubakaji unaofanywa namagenge ya watu.
Watu wengi waliolazimika kuyaacha makaazi yao wanaishi katika maeneo ya wazi anasema Linsay Hamsik mshauri wa masuala ya sera katika muungano wa mashirika kiasi 300 yasiyo ya kiserikali na mashirika ya msaada ya Kimataifa nchini Sudan Kusini.
Hamsik anasema kinachodhihirika nchini humo kwa sasa ni kutokuwepo kwa nia ya kisiasa katika kuutatua mgogoro na hicho ndicho kiini kinachosababisha maisha zaidi ya watu kupotea na raia kuendelea kufanyiwa unyama na hata kunyimwa haki zao za kupata msaada.Kwa mujibu wa Hamsik kwa hivi sasa maeneo yanayokabiliwa na vita vikali ni Jimbo la Unity ambalo ni eneo muhimu lenye utajiri wa mafuta.
Utekaji nyara wa watu wengi unaripotiwa mara kwa mara sambamba na vitendo vya wanawake na watoto kubakwa.Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya na Marekani zilitoa taarifa ya kutaka pande zote zinazohasimiana kuondoa vipingamizi vinavyoyazuia mashirika ya kutoa misaada kuwafikia wanaohitaji msaada.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Daniel Gakuba